Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 08:43

Waziri wa fedha wa Tanzania awalaumu wafadhili, asema masharti mengi ni ovyo


Waziri wa Fedha Dkt Philip Mpango
Waziri wa Fedha Dkt Philip Mpango

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango, amesema nchi inapita kwenye kipindi kigumu baada ya wafadhili kupunguza misaada na ameeleza kuwa ile iliyobakia imekuwa na masharti yakiwemo ya kukubali ushoga ambayo ni ovyo kabisa.

“Mtakuwa mmesikia jinsi ambavyo sasa wanafika mahali, hata bila aibu, wanasema sisi tuvumilie ushoga, Mnakubali? Mnakubali niende kuomba hela ya nchi halafu kuchekelea ushoga hata mbuzi hawafanyi?

“Tukipeleka jeshi letu kudhibiti magendo, wanasema tunarudisha nyuma biashara ya usafirishaji hapa nchini. Inawezekana? Kwa hiyo ninachotaka kuwaambia ni nini? Marehemu Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere) alitufundisha kwamba tumepata uhuru wa bendera, lakini tuna kazi ya kutafuta uhuru wa kiuchumi,” Waziri alisema.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimeripoti kuwa Waziri huyo aliongeza kuwa:“Sasa hapo ndipo shughuli pevu lazima tujitegemee na ili tujitegemee serikali kuu, serikali za mitaa lazima zijielekeze kukusanya mapato ya ndani ndiyo maana yake hakuna nyingine.”

Dkt Mpango alisema serikali ikidhibiti madini wanasema wanafukuza wawekezaji na kwamba wamechukua miaka 57 sasa inatosha.

“Ninachotaka kuwaambia salamu zangu, kila Mtanzania popote alipo hasa nyie mliomo humu ndani kila mtu aweke Tanzania moyoni mwake. Ni lazima kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa nguvu zote na hasa kwa kutumia mfumo huu wa GePG (wa njia ya kielektroniki), lazima twende kisasa,” alisema.

Amesema anaamini mfumo huo utasaidia kupata mapato yote stahiki kwa ajili ya kuendesha serikali kuu na serikali za mitaa.

“Hakuna mjomba, mjomba anayekutakia ya ovyo ovyo namna hiyo hapana ‘enough is enough’ (inatosha). Kama mnaipenda Tanzania kila mtu akazane na kusimamia huo mfumo to the best of ability (kwa uwezo wake). Mzingatie mafunzo mnayopata, mzingatie sheria zote, tunaelewana? Nawasihi sana,” alisema.

“Utumwa sasa mwisho lazima tutembee kifua mbele. Mzingatie mafunzo haya kwenye kazi zenu ili tujidai sasa ni taifa huru linalojiendesha lenyewe,” alisema huku akisisitiza kuwa anatamani katika bajeti ijayo, Tanzania ijitegemee bila kukopa.

“Mungu atakaponipa nafasi nisimame nitamke kuanzia sasa serikali yetu itajitegemea tutatafuta mikopo labda ya kibinadamu kama matetemeko na mafuriko, hiyo ndiyo tutaenda kutafuta nje lakini vinginevyo tufanye wenyewe na tunaweza,” alisisitiza.

XS
SM
MD
LG