Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 08:59

Tanzania yatakiwa kutekeleza masharti ya Benki ya Dunia


Benki ya Dunia (WB) Kanda ya Afrika, imesema kuwa serikali ya Tanzania imetakiwa kutekeleza masharti ya benki hiyo kabla haijapewa mkopo wa Dola 300 milioni za Marekani kwa ajili ya kuboresha elimu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt Hafez Ghanem alisema benki yake inatoa fedha kwa ajili ya wasichana wote bila kuwatenganisha kwa kigezo cha ujauzito .

Gazeti la Mwananchi nchini Tanzania limemnukuu akisema: "Mradi wa Tanzania haujajadiliwa. Lakini kwa mazungumzo tuliyofanya, utajadiliwa Serikali itakapotimiza masharti tuliyokubaliana."

Baada ya mazungumzo yaliyo fanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais John Magufuli alisema benki imekubali kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara, nyumba za walimu na vifaa vya kufundishia.

Awali chanzo ndani ya benki hiyo kiliiambia BBC Swahili kuwa sababu kuu mbili za zuio hilo zilikuwa ni mosi, uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuzuia wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo mara baada ya kujifungua.

Pili, maboresho ya Sheria ya Takwimu yaliyo pitishwa na Bunge la Tanzania Septemba 10 ambapo pamoja na mambo mengine, inakataza usambazaji wa takwimu zinazolenga kupinga, kupotosha au kukinzana na takwimu rasmi za serikali.

Adhabu ya kukaidi sheria hiyo ni faini ya Dola 6,000 au kwenda jela miaka mitatu.

Aidha Dkt Ghanem alisema walizungumzia mabadiliko ya Sheria ya Takwimu na wameishauri Serikali kuhakikisha wadau wake wanakuwa huru kukusanya na kutumia takwimu.

Siku ya Ijumaa Rais Magufuli alisema pesa hizo "hazijafyekelewa mbali" kama baadhi ya watu "wasiotutakia mema walivyosema."

Rais Magufuli alinukuliwa akisema kuwa Ghanem alikwenda Tanzania kuthibitisha kuwa Benki ya Dunia haitaiacha nchi hiyo.

XS
SM
MD
LG