Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 07:18

CPJ yakanusha taarifa ya uhamiaji Tanzania


Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania, imewaachia huru na kuwarudishia hati za kusafiria waandishi wa Kamati Maalumu ya Kuwalinda Wanahabari Duniani (CPJ), na kudai kuwa waliingia nchini na kufanya shughuli zao kinyume na kibali cha matembezi walichokuwa wamepewa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyo tolewa na Msemaji wa Idara hiyo, Ally Mtanda, wafanyakazi hao Angela Quintal ambaye ni raia wa Afrika Kusini na Mumo Muthoki, raia wa Kenya walikuwa na kibali cha matembezi (holiday visit) cha miezi mitatu ambacho kinaisha muda wake Januari Mosi, mwaka 2019.

CPJ yasisitiza ilifuata sheria

Lakini msemaji wa CPJ yenye makao yake makuu mjini New York, amekanusha kuwa wafanyakazi hao walikuwa nchini bila kibali cha kufanya shughuli. Jonathan Rozen amesema Alhamisi Quintal na Muthoki walifuata utaratibu wa kawaida wa kuomba visa na walikuwa nchini Tanzania kwa kufuata sheria.

“Kabla ya timu hii kuondoka kwenda Tanzania CPJ ilizungumza na serikali ya Tanzania juu ya utaratibu unaotakiwa kufuatwa kabla ya kuingia nchini na walikuwa wamekidhi matakwa yote ya serikali. Walikuwa na vibali vyote vinavyo hitajika kuingia nchini; visa zinazoruhusu wao kuingia na kufanya shughuli zao za kikazi.”

Kwa mujibu wa msemaji huyo kauli ya serikali “ imewashangaza CPJ sana” kwa sababu CPJ ilifuata utaratibu wa kisheria wa kujua nini kilikuwa kinahitajika na kutekeleza.

Kuongezeka wasiwasi Tanzania

Amesema kumeendelea kuwa na wasiwasi mkubwa kwani kukamatwa kwa waandishi wa habari na kufinywa kwa uhuru wa habari, magazeti, mitandao ya kijamii unaotokana na sheria na masharti ya kuchapisha habari mitandaoni zilizopitishwa.

“Mwezi Mei 2018 tuliungana na taasisi nyingine 64 tukaeleza sikitiko letu juu ya kupungua kwa uhuru wa vyombo vya habari Tanzania. Pia athari za ukandamizaji huo ambao unawaathiri waandishi wa habari Tanzania.”

“Tunapokwenda katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kazi zetu za kuwalinda waandishi wa habari, lengo ni kufahamu vizuri zaidi hali ya uhuru wa habari ilivyo katika nchi hizo na kutafuta njia za kuboresha uhuru wa habari katika nchi hizo. Pia lengo ni kufahamu hali ya uhuru wa habari nakujenga mahusiano bora zaidi na vyombo vya habari.

Juhudi zilifanyika

Mara baada ya kupata taarifa za kukamatwa kwao tulijaribu kwa bidii yote kuwasiliana na serikali ya Tanzania na ubalozi wa Tanzania nchini Marekani lakini bila mafanikio yoyote.

Amesema hivi sasa CPJ wanajaribu kuwasaidia wafanyakazi hao kupata mapumziko baada ya kufikwa na misukosuko hiyo wakati wa ziara yao nchini Tanzania.

Rozen ameongeza kusema kuwa CPJ inatafakari tukio hili la kukamatwa kwa wafanyakazi wake na kujaribu kuangalia kwa undani lina maana gani kwa uhuru wa vyombo vya habari Tanzania.

“Hii ni ishara gani kwa vyombo vya habari na jumuiya ya waandishi wa habari diniani na nini taswira ya Tanzania kwa ulimwengu juu ya suala zima la uhuru wa vyombo vya habari.

Madai ya uhamiaji

Taarifa hiyo ya Uhamiaji imesema baada ya mahojiano, wafanyakazi wa CPJ walikiri wameingia nchini kwa lengo la kufanya vikao na waandishi wa habari nchini wakati vibali vyao ni kwa ajili ya matembezi kinyume na Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54, na kanuni zake za viza za mwaka 2016.

Hata hivyo, baada ya uchunguzi idara hiyo imewaachia huru na kuwarejeshea hati zao za kusafiria kwa masharti ya kutoendelea na vikao hivyo kwa kutumia vibali vya matembezi walivyopewa.

Waandishi hao wanadaiwa kukamatwa katika Hoteli ya Southern Sun jijini Dar es Salaam na kushikiliwa hati zao za kusafiria na kisha kuachiwa huru.

XS
SM
MD
LG