Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 07:16

Serikali ya Tanzania yawaachia huru wafanyakazi wa CPJ


Muthoki Mumo (kushoto) na Angela Quintal
Muthoki Mumo (kushoto) na Angela Quintal

Vyombo vya Dola nchini Tanzania Alhamisi vimewaachia huru Wanaharakati wa CPJ (Kamati Maalum ya Kuwalinda Wanahabari duniani) Muthoki Mumo na Angela Quintal ambao walikuwa wanashikiliwa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Uingereza BBC Idara ya kimataifa ya uhusiano na ushirikiano nchini Afrika Kusini (DIRCO) ilisema waandishi hao sasa wamerudi kwenye hoteli yao.

"Balozi wa Afrika Kusini Bw Thami Mseleku amekutana nao na kuzungumzia kile kilichotokea. Kisha atazungumza na mamlaka za Tanzania. Msemaji wa DIRCO Bw Ndivhuwo Mabaya, alizungumza na Bi Quintal leo asubuhi," Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya Afrika Kusini ilisema kwenye mtandao wa Twitter.

Taarifa iliyotolewa na Kamati hiyo, imeitaka Serikali kuwaachia mara moja Kiongozi Mkuu wa Kamati hiyo Afrika, Angela Quintal na Mwakilishi wa Afrika Mashariki Muthoki Mumo na kuwarudishia hati zao za kusafiria ambazo walizichukuwa bila ya kufuata utaratibu.

Imeeleza kuwa wanaharakati hao walikamatwa na watu waliojitambulisha wanatoka Idara ya Uhamiaji, wakiwa katika Hoteli waliyofikia jijini Dar es Salaam, Jumatano jioni na kuwapekua kisha kuchukua hati zao za kusafiria na kugoma kuzirejesha.

Baada ya kupekuliwa na kupokonywa pasipoti zao, viongozi hao walitolewa kutoka kwenye hoteli na kupelekwa kusikojulikana, imeongeza.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa wanaharakati hao waliwasili nchini ili kuripoti katika majukumu yao.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vinasema kuwa mara baada ya kukamtwa Quintal na Mumo ujumbe wa twitter ulitumwa kutoka akaunti ya Quintal, ukisema "Mungu ni mkuu tumeachiliwa na tunarudi hotelini," na kuzua hofu kuwa mtu fulani alitumia simu zake.

"Ujumbe wa @angelaquintal haukutumwa naye," aliandika mpwa wake Quintal, Genevieve Quintal, ambaye pia ni mwandishi wa habari. "Hii inaonyesha kuwa kuna mtu anatumia simu yake."

Akaunti za Twitter za Quintal na Mumo zimezimwa tangu wakati huo.

XS
SM
MD
LG