"Maagizo hayo yalipaswa kutekelezwa ndani ya siku 30, lakini leo tunapoongea hapa, siku hizo zimekwisha, napenda kuwajulisha kuwa mwitikio umekuwa wakuridhisha, lakini tunatoa muda huo wa siku 14 kwa NGO zilizobaki kukamilisha agizo hilo," Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt John Jingu amesema.
Hapo awali serikali kupitia Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile katika kikao chake na waandishi wa habari Septemba 28, mwaka huu alitoa muda wasiku 30 kwa NGO kuhakikisha zinapeleka taarifa hizo wizarani kwake.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa Dkt Jingu alisema kutokana na agizo hilo baadhi ya mashirika hayo yameshindwa kukamilisha kwa wakati na kuomba muda zaidi wa kumaliza kutayarisha taarifa zao.
Alisema serikali imekubali ombi lao la kuongezewa muda na kutoa muda wa siku 14 kwa mashirika hayo yaliyobaki kuhakikisha wanakamilisha taarifa zao kwa wakati uliobaki baada ya hapo sheria itafuata mkondo wake.
Aliyataja maagizo yaliyo tolewa na serikali kuwa ni kuhakikisha wanawasilisha taarifa zao za fedha zilizokaguliwa za mwaka 2016 na 2017.
Maagizo mengine ni mashirika hayo kuwasilisha taarifa za kazi za mwaka 2016/2017, kuwasilisha mikataba ya ufadhili ya miaka hiyo miwili pamoja na kuwasilisha vyanzo vyote vya fedha na matumizi yake.
Taarifa zingine walizotakiwa kuziwasilisha ni kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa inazingatia vipaumbele, mipango na mikakati ya serikali katika ngazi ya taifa, mikoa, wilaya ili kutoa mchango katika kufikia maendeleo endelevu kwa manufaa ya jamii na taifa.
Masharti mengine yaliyotolewa kwa NGO hizo ni kuhakikisha kabla ya kutekeleza miradi yao sharti wawasiliane na Ofisi ya Msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali na Ofisi ya Rais Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili kufanikisha jukumu la uratibu.
Agizo hilo limesema mashirika hayo ambayo hayakusajiliwa RITA, BRELA na Wizara ya Mambo ya Ndaniya Nchi, yanayofanya shughuli za kijamii, yalitakiwa kutekeleza matakwa ya sheria ya NGO ya kuomba cheti cha ukubalifu.
Alisema serikali inatambua na kuthamini mchango wa NGO kwa maendeleo ya nchi, lakini kinachotakiwa ni uwazi na uwajibikaji kwa maendeleo mazuri zaidi.
Wizara inaeleza kuwa uwazi na uwajibikaji utasaidia kuzuia matumizi mabaya ya rasilimali zinazotolewa na wadau wa maendeleo kupitia mashirika hayo yasiyokuwa ya kiserikali.
Akitoa sababu ya serikali kufanya hivyo, alisema ni kutokana na baadhi ya mashirika hayo yasiyokuwa ya kiserikali kuingiliana kwenye utekelezaji wa miradi yao na wengine kutoeleweka kazi zao wanazo fanya kwenye Jamii na fedha walizoomba kuishia mifukoni mwao.