Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 15:24

Wakili wa Abdul Nondo asema polisi walimzuia kinyume cha sheria


Abdul Nondo
Abdul Nondo

Wanasheria ambao wanamtetea Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi nchini Tanzania (TSNP), Abdul Nondo wanasema kuwa polisi walikuka sheria walipomshikilia mteja wao bila ya kumfikisha mahakamani kwa siku 20 mwezi huu.

Polisi wa Tanzania walimtia nguvuni kiongozi huyo wa wanafunzi Machi 7 baada ya kudai kuwa ametekwa lakini baadaye akapatikana mjini Iringa, kusini mwa nchi hiyo.

Katika mahojiano maalum na Sauti ya Amerika, wakili Reginald Martin anayewakilisha jopo la mawakili wenzake katika shauri hilo amesema “Sheria haikufuatwa, kwa sababu utaratibu wa sheria unawalazimisha polisi kumpeleka mahakamani mtuhumiwa katika kipindi cha masaa 24 au kutokaa naye zaidi ya masaa 24 lasivyo kumpa dhamana kama inaonekana haiwezekani kumfikisha mahakamani ndani ya masaa 24."

Wakili huyo anasema hatimaye mteja wao Abdul Nondo alirejeshwa Iringa ambako ndiko alikopatikana na kufunguliwa mashitaka lakini akanyimwa dhamana.

Wakili Martin amesema pia kuwa hakupata taarifa za mapema za kufikishwa mahakamani kwa mteja wake na juhudi za kumwombea dhamana hazikufanikiwa ingawa watu wa kumdhamini walikuwepo.

“Mvutano wa hoja ulijitokeza hapo mahakamani ambapo mwendesha mashtaka wa serikali alipinga Nondo kupewa dhamana akisema ni kwa ajili ya usalama wake mshtakiwa,” amesema Wakili Martin.

Kufuatia tukio hilo mawakili wanaomtetea Nondo wamefungua maombi mahakama kuu Dar es Salaam wakitaka Mkuu wa Mkurugenzi wa makosa ya jinai, Inspekta Jenerali wa Polisi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wajibu hoja ya kwa nini Nondo amenyimwa dhamana.

Abdul Nondo ambaye pia ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) aliripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha lakini baadaye akapatikana akiwa hai eneo la Mafinga mkoani Iringa.

Mwigulu Nchemba -Michuzi blog
Mwigulu Nchemba -Michuzi blog

​Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba alimwambia Rais John Magufuli Machi 11, 2018 akiwa mkoani Singida "...ndiyo maana unaona vinyago vingi vingi hivi kama hivi juzi anatokea kijana mdogo eti anasema ametekwa, eti ametekwa akapata na muda wa kutafuta perfume na nguo za kubadilishia kule atakakokuwa ametekwa, unaotoa wapi muda wa kujiandaa ni vitu vya kiajabu ajabu kama hivyo watu wanatafuta namna za kuchafua taswira za nchi yetu na jambo hili si jambo ambalo tutacheza nalo.”

Mkuu wa Mkoa Paul Makonda
Mkuu wa Mkoa Paul Makonda

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda aliwaamrisha Polisi wa Mkoa wa Iringa wakimalizana na Abdul Nondo aliyedaiwa kupotea kisha kupatikana mkoani Iringa, arejeshwe Dar es Salaam kwa maana ameuchafua mkoa huo.

Aidha, aliwataka waandishi wa habari nchini Tanzania waangalie taarifa wanazopeleka kwa umma, kama hazijathibitishwa na mamlaka husika waachane nazo.

XS
SM
MD
LG