Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 02:17

Malecela avinasihi vyombo vya usalama kujitathmini


Waziri Mkuu mstaafu John Malecela
Waziri Mkuu mstaafu John Malecela

Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela ameshangaa vyombo ya dola kushindwa kujipanga sawasawa na kukumbusha umuhimu wa kujitathmini.

Malecela alikuwa akitoa tathmini yake kuhusu kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Afrika na duniani, Mohammed Dewji maarufu pia kwa jina la Mo na matukio mengine kadhaa ya namna hiyo yaliyo kwisha tokea nchini Tanzania.

Katika mahojiano na gazeti la Mtanzania alishangaa vyombo vya dola kushindwa kujipanga kwa kadiri maendeleo yanavyokua na uhalifu unavyo ongezeka.

Alisema vyombo hivyo vilipaswa kutambua miaka mitano iliyopita kwamba ipo siku taifa litafikia katika kiwango hiki cha uhalifu wa watu kupotea, kutekwa nyara au kujeruhiwa na watu wasiojulikana.

Malecela alisema kama haitoshi haipaswi taifa kila siku kikitokea kitu kipya watu washangae, badala yake uwekwe utaratibu madhubuti wa kufanya tathmini ya kila siku kuangalia mbele zaidi usalama wa raia.

“Hivi kweli kwa vyombo vya usalama, miaka mitano iliyopita havikujuwa kwamba tutafika hapa? Kwamba Tanzania itakuwa na wahalifu kama Nigeria, ambako wahalifu 20 au 30 wanaweza kuvamia mtaa, wakateka watu nyara au wakachukuwa vitu na kutoweka chini ya nguvu ya mtutu?” alihoji Malecela.

Alisema mtazamo wake ni kuwa vyombo vya usalama lazima vifanye tathmini juu ya mambo yajayo na kujitayarisha kwa sababu uhalifu unaotokea hapa nchini hauwezi ukatajwa kuwa si wa kawaida, kwamba haujawahi kutokea duniani.

Malecela ambaye amepata kuhudumu katika nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia Serikali ya awamu ya kwanza na zaidi akiwa Waziri Mkuu kwa takribani miaka minne (1990-1994) katika Serikali ya awamu ya pili chini ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alisema vyombo vya usalama vilipaswa kusoma alama za nyakati miaka mitano iliyopita.

“Hatuwezi kukaa na kuanza kuomboleza kutekwa watu nyara, tuliona wenzetu Kenya mambo haya yalianza siku nyingi wakina Kariuki (Josiah Mwangi Kariuki, mwanasiasa na mmoja wa viongozi mara baada ya Kenya kupata uhuru) walipotea hivi hivi.

“Kenya wanasiasa wengi walipotea hivi hivi, watu kuuawa,mfano marehemu Tom Mboya (Waziri wa zamani wa Kenya na mwanasiasa machachari wa Kanu), haya yalikwisha tokea kwa nini yasitokee na Tanzania?

“Kama uhalifu huu upo lazima tujitayarishe na ninatoa pole kwa wenzetu ambao wamepoteza watoto wao na ndugu zao na pia nasikitika sana, lakini ni mambo ambayo yatatokea na yataendelea kutokea.

“Kwa upande wa Jeshi la Polisi wasipopata msaada wa raia watakuwa na wakati mgumu kudhibiti uhalifu, kwa sababu raia hao hao wanaopiga kelele kulaumu polisi ndio unakuta hao hao wamehifadhi wahalifu,” alisema Malecela.

XS
SM
MD
LG