Vurugu za kisiasa Indonesia zaua watu sita, 200 wajeruhiwa

Polisi wakipambana na waandamanaji wanaodaiwa walikuwa wanafanya vurugu mjini Jakarta, Indonesia, Mei 22, 2019.

Rais wa Indonesia Joko Widodo amesema hawezi kuvumilia kuona mtu yeyote anavuruga mchakato wa kidemokrasia wa nchi hiyo, baada ya mapambano ya hatari kati ya polisi na wafuasi wa Prabowo Subianto, jenerali mstaafu wa jeshi aliyeshindwa katika uchaguzi hivi karibuni.

Gavana wa Jakarta amesema watu wasiopungua sita wameuawa na wengine zaidi ya 200 wamejeruhiwa katika vurugu hizo Jumatano.

“Hatutatoa fursa yeyote ghasia kufanyika, hasa wale ambao wataleta uharibifu wa nchi ya Indonesia,” hivi karibuni Rais aliyechaguliwa tena Widodo aliwaambia waandishi, akiongeza kuwa jeshi na polisi watachukuwa hatua madhubuti kwa kufuata sheria.

Vyombo vya usalama vimeeleza kuwa waandamanaji walikaidi kutawanyika wakati polisi walipokuwa wanajaribu kuwashawishi kuondoka wakiwaambia ni mwezi wa Ramadhani na wajiepushe na kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani katika mwezi mtukufu. Waandamanaji waliamua kuchoma nyumba ya malazi ya polisi na magari. Polisi hatimaye walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji.

Msemaji wa Polisi Dedi Prasetyo ameiambia VOA kuwa maandamano hayo yalibadilika kuwa vurugu Jumanne usiku na vurugu hizo kuendelea hadi mapema Jumatano. Darzeni za watu wamekamatwa.

Widodo amesema hali hivi sasa iko shwari chini ya ulinzi wakati akiwataka wananchi wa Indonesia kuungana baada ya uchaguzi.

Tume ya Uchaguzi ya Indonesia Jumanne imethibitisha kuwa Joko Widodo, ambaye anajulikana pia kama Jokowi, alichaguliwa tena kwa kura asilimia 55.50, na kumshinda jenerali mstaafu wa jeshi Prabowo.Ushindi huo ulithibitshwa na Tume ya Uchaguzi Mkuu (KPU).

Prabowo, mgombea kwa mara ya nne ambaye ananasibishwa na wanasiasa wasomi na Waislam wenye msimamo mkali, alipata kura asilimia 44.50.

Prabowo ametoa tamko kupitia picha ya video Jumanne, akihimiza wafuasi wake kumuunga mkono kwa njia ya amani.

"Hatua zetu lazima zifuate katiba, demokrasia, amani bila ya vurugu! Wale wote waliokuwa na imani na mimi na marafiki zangu hapa… hatupiganii maslahi binafsi, lakini kwa ajili ya uhuru wa watu wetu, kwa ajili ya demokrasia, kwa ajili ya Indonesia huru, ili tuwe huru kutokana na uvamizi wa nchi yetu katika muundo wowote,” amesema.

Prabowo amekataa kukubali matokeo na kutangaza kuwa yeye ndiye mshindi. Katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari Jumanne asubuhi, amesema kuwa timu ya kampeni yake imepanga kupinga matokeo ya uchaguzi katika Mahakama ya Katiba. Anadia kulikuwa na wizi mkubwa wa kura lakini hakutoa ushahidi wowote wa kuthibitisha hilo.

Msemaji wa Polisi mjini Jakarta, Argo Yuwono, ameiambia VOA kuwa askari wasiopungua 50,000 walikuwa wamepelekwa katika eneo hilo ikitarajiwa kutokea fujo zilizokuwa zimeandaliwa.