Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Januari 24, 2025 Local time: 08:50

Uamuzi wa Trump waibua hasira ulimwengu wa Kiislam


Wapalestina wakikabiliana na majeshi ya Israel wakati wa maandamano ya kupinga uamuzi wa Rais Trump kuitambua Jerusalem kuwa makao makuu ya Israel.
Wapalestina wakikabiliana na majeshi ya Israel wakati wa maandamano ya kupinga uamuzi wa Rais Trump kuitambua Jerusalem kuwa makao makuu ya Israel.

Makundi makubwa ya waandamanaji katika ulimwengu wa Kiislam wamefanya maandamano likiwemo eneo la Gaza Ijumaa baada ya Marekani kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel na Mpalestina amepoteza maisha baada ya kupigwa risasi huko Gaza.

Mpalestina huyo, Mahmoud al-Masri, miaka 30, aliuawana askari wa Israel wakati wa mapambano kwenye mpaka wa Gaza- Israel baada ya Wapalestina kutaka iwepo “siku ya hasira” kupinga kitendo hicho cha Marekani.

Jeshi la Israel limethibitisha kuwapiga risasi watu wawili katika eneo la Khan Yunis huko Kusini mwa Gaza, wakiwatuhumu kuwa ndiyo “wachochezi wakuu” wa vurugu zilizokuwa na uvunjifu wa amani.

Ndege za kivita za Israel pia zilipiga maeneo ya kijeshi ya Hamas katika eneo la Gaza kujibu shambulizi la roketi iliyokuwa imerushwa kutoka eneo hilo. Wizara ya afya ya Palestina imesema kuwa siyo chini ya watu 15 walijeruhiwa wakati ndege za Israel ziliposhambulia.

Waandamanaji walijitokeza Ijumaa huko Iraq, Jordan, Syria, Pakistan, Lebanon, Malaysia, na Indonesia, nchi zenye idadi kubwa ya Waislam walio wengi duniani kuonyesha kukasirishwa kwao juu ya maamuzi hayo yaliyofanywa na Marekani.

Waandamanaji wamechoma matairi na kurusha mawe huku maafisa usalama wa Israel wakiwatupia mabomu ya machozi wandamaanaji hao na risasi za mpira.

Taarifa za vyombo vya habari zinasema kuwa upande wa Gaza kundi la Hamas limetangaza intifada au mapambano dhidi ya maamuzi hayo ya Rais Trump.

Omary Shakir ambaye ni mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch katika eneo la Isreal na Palestina yupo mjini Ramala, ameiambia BBC kuwa baada ya Israel kuwepo katika eneo hilo kwa miongo kadhaa sasa Wapalestina wengi wamekuwa na hasira na tangazo la Rais Trump.

Kwa upande wake Naibu waziri anayehusika na masuala ya Diplomasia wa Israel Michael Oren ameimbia BBC kuwa tangazo la Rais Trump limeifanya iwe siku ya furaha kwa kwa taifa la Israel na Israel ilitarajia vurugu kutoka kwa wapalestina.

Umoja wa Nchi za Kiarabu, ambazo zinajumuisha takriban dazeni mbili za mataifa mbalimbali, zinakutana Jumamosi katika juhudi za kuchukua msimamo wa pamoja juu ya uamuzi wa Marekani kuitambua Jerusalem.

Vyanzo vya habari vimeripoti kuwa Marekani imeionya Palestina dhidi ya maamuzi yake ya kutotaka kukutana na makamu wa rais wa Marekani Mike Pence katika kikao ambacho kilipangwa kufanyika mapema mwezi huu.

Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza Jumatano kuwa Jerusalem ni mji mkuu wa Israel na Marekani inafanya mchakato wa kuhamisha ubalozi wake katika mji huo.

Israel inaamini kuwa sehemu yote ya Jerusalem kuwa ni makao yake makuu. Wapalestina wanataka upande wa mashariki wa Jerusalem uwe makao yao makuu ya taifa huru litakapopatikana siku za usoni.

XS
SM
MD
LG