Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 23:06

Wanaharakati wadai walisumbuliwa wakati wa mkutano wa SADC Tanzania


Rais John Magufuli
Rais John Magufuli

Wanaharakati wa jumuiya za kiraia za Afrika waliohudhuria mkutano walihojiwa na kuonywa na polisi wa Tanzania mwisho mwa wiki katika kile wanaharakati wa haki za kibinadamu wanachosema ni kuendelea kukandamizwa kwa uhuru wa kujieleza katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Maelezo zaidi yanaendelea kuibuka kuhusu yaliyowapata wafanyakazi wa jumuiya za kiraia zipatazo 40 ambao walidaiwa kuwa kinyume na matakwa ya maafisa wa usalama wa Tanzania walipokusanyika jijini Dar es Salaam kuhudhuria Mkutano wa mwaka huu wa jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC.

Lakini wataalamu wa haki za binadamu wamesema Jumatatu kuwa tukio la mwisho wa wiki hii ni ishara tosha inayoleta wasiwasi juu ya serikali ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki kuzidi kuwa na hofu na kuendeleza unyanyasaji.

Catherine Eden, Wakili wa Muungano wa watetezi wa Haki za Binadamu, anasema tukio hilo lilitokana na kutoelewana baina ya wanaharakati na maafisa usalama.

Wajumbe wa Afrika Kusini kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na mataifa 16, wamesema walitaka kuadhimisha August 16 mauaji yaliyotokea katika machimbo ya Marikana Afrika Kusini. Lakini kitu walichokuwa wameandika katika karatasi kiliwafanya polisi wafikirie kuna mpango mkubwa zaidi.

"Waliandika baadhi ya ujumbe katika makaratasi, kati ya maandishi hayo, baadhi yalisomeka, "Acheni kuwaua watu wetu." ...Kwa hiyo nafikiri kulikuwa na mtu wa usalama wa taifa katika mkutano huo na alivyoona ujumbe huo akatafsiri kuwa ni mpango wa kuandamana."

Janet Zhou, mkurugenzi wa muungano wa Zimbabwe wa kusimamia madeni na maendeleo, alikuwa mmoja wa wanakampeni waliohojiwa na vikosi vya usalama. Alizungumza na VOA aliporejea Harare, na kusema ilikuwa ni tukio la kufadhaisha.

"Nilikuwa nimetishika, sikuwa na amani, nilipatwa na hofu kwa kifupi. Kwa sababu maafisa wa usalama saba walikuja baada ya saa sita za usiku na kunihoji juu ya maandamano na mabango ambayo sikuwa na njia ya kuwapatia, ilikuwa suala jingine. Sikufahamu chochote. Iliniacha katika hali ya mshtuko mkubwa.

Amesema polisi baadae walimtaka yeye -- na ujumbe wake wa watu 40 -- wabakie hotelini siku yote ya Jumamosi. Aliwauliza iwapo wako chini ya ulinzi, jambo ambalo hawakujibu.

Anna Henga, Mkurugenzi wa kituo cha sheria na Haki za Binadamu, amesema vitendo vya polisi vinaendeleza tu kuwepo kwa hali ya wasiwasi nchini Tanzania, chini ya utawala wa Rais John Magufuli ambaye wakosoaji wake wanasema anazidi kuwa mkandamizaji.

"Hii inamaana ni kuendelea kuminya harakati za kiraia. Kwa sababu hili limeanza kufanyika tangu 2016. Kuna masuala mengi sana, kuna matokeo hasi katika kuendelea kuminywa uhuru wa kiraia. Na unalenga watu kama vile jumuiya za asasi za kiraia, vyombo vya habari, ikiwemo kuzuia uhuru wa kujielezea, na uhuru wa kukusanyika."

Eden alieleza masikitiko yake, kama walivyoeleza makundi ya kimataifa kama vile Kamati ya Kuwalinda Wanahabari (CPJ), ambapo kabla ya kuanza mkutano wa SADC ilieleza hofu yake juu ya "hali inayotia wasiwasi mkubwa ya kutoweka kwa uhuru wa habari" nchini Tanzania.

Waangalizi hao wa CPJ walimtaja hasa mwandishi wa Tanzania Azory Gwanda, ambaye alitoweka tangu 2017, na Erick Kabendera, aliyekamatwa mwezi Julai na kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi, jambo ambalo linaelezwa na CPJ ni kulipiza kisasi kwa uandishi wake unaoikosoa serikali.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Afrika Kusini

XS
SM
MD
LG