Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:28

Mkutano wa Watanzania, Washington : Lissu ataka wauaji wote wawajibishwe


Tundu Lissu akiwasili katika mkutano wake na Watanzania wanaoishi Marekani, Februari 9, 2019.
Tundu Lissu akiwasili katika mkutano wake na Watanzania wanaoishi Marekani, Februari 9, 2019.

Mnadhimu wa Kambi ya upinzani katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye yuko ziarani nchini Marekani na ulaya amesema kwa sababu serikali ya Tanzania imevunja (our obligation to the world) "jukumu letu kwa dunia, ni wajibu wetu kuueleza uovu huo kwani dunia inahaki ya kujua hilo.”

Amesema : “Ninataka wauaji wote wawajibishwe, hayo ni majukumu yetu kwa ulimwengu, tunapovunja majukumu yetu ya kuzuia kuuawa na kukandamizwa wananchi wetu, jumuiya ya kimataifa haina jukumu kutusaidia kwa chochote, hata senti moja.”

“Hatuwezi kuacha tuwe taifa lenye kikosi cha mauaji,” akifafanua baadhi ya matukio ya kutisha yaliyotokea nchini Tanzania.

Amesema Tanzania imekuwa serikali ya "kupoteza watu", hakuna tofauti na serikali ya Iddi Amin, iliyokuwa inapoteza watu nchini Uganda.

Mauaji Rufiji

Mbunge Lissu pia amehoji nani waliohusika huko Rufiji, Kilwa, Mkuranga na Kibiti ambapo raia waliochukuliwa kutoka misikitini, mashambani na majumbani wametoweka hadi leo. Pia aligusia nani aliyewateka Mohamed Dewji, Roma Mkatoliki, Azory Gwanda, Ben Sanane na wengine.

Pia amewataja watu wawili Mohamed Mruttu na Abdallah Bushiri ambao alikutana nao Central Police Dar es Salaam, wakati alipokamatwa na kuwekwa rumande katika kituo hicho maarufu kama shimoni Juni 29, 2016.

Amedai watu hao walikuwa wamekaa rumande hapo, mmoja kwa kipindi cha miezi miwili na nusu na mwengine takriban miezi minne.

Watu hao walipoletwa kwake na mahabusu wenzao walikuwa wanamtaka Lissu awasemee kwa RPC Salum Hamduni.

“Mheshimiwa kwa sababu umekuja hawa mabwana wawili tunaomba ukawasemee, wamekuwa vilema, wanateswa,” Lissu alisema.

Kikosi maalum au task force

“Watu hao walikuwa wamepigwa hawafai, wanachukuliwa usiku, kuna kitu kinaitwa task force (kikosi maalum) ukikutana na mtu akikuambia habari za task force hutatamani kusikia.

Nikamwambia sasa afande Salum si unanipeleka mimi leo mahakamani Kisutu, nikitoka Kisutu kitu cha kwanza nitakachokisemea na nilikisemea ni “kwa nini serikali hii inatesa watu,” alisimulia Lissu.

Baada ya siku mbili tatu Lissu alikutana na vijana hao mahakamani, alipokuwa amekwenda kuwatoa vijana waliokamatwa na polisi kwa kurusha meseji mitandaoni na kuwekwa mahabusu kituo cha polisi Oysterbay.

Abdallah alimwambia Lissu kwamba ameshtakiwa kwa kuwa na nyara za serikali na Mruttu alisema ameshtakiwa kwa ugaidi.

Watu hao walieleza kuwa wakati wote huo walikuwa wanachukuliwa usiku, wanapelekwa mahali fulani eneo la Mikocheni Dar es Salaam, wanateswa na wanarudishwa Alfajiri wanavuja damu, hawafai.

Pia Lissu amesema alikuwepo Msanii Wema Sepetu ambaye tayari alikuwa ndani kwa wiki mbili hapo rumande shimoni. Pia ameongeza kuwa kulikuwa na wasichana kutoka Burundi ambao walikuwa wamekaa kwa takriban wiki tatu.

Lissu ameuliza: “Mnataka muungwe mkono mnapouwa watu wenu. Kama hilo ni sawa tukubaliane? Lakini naamini hilo sio sawasawa.”

Lissu amesema hata kama atabaki peke yake kwa sababu wengine wanaogopa kusema ataueleza ulimwengu juu ya nchi yenye matendo ya kutisha yasiyojulikana, ambayo yanatokana na utawala wa Rais Magufuli. Lakini amesisitiza kuwa “tukiwa wengi (tunalieleza hili) itakuwa vizuri.”

“Jukumu langu sio tu kueleza jaribio la mauaji yangu peke yake,” amesema.

Watanzania wajitokeza kwa wingi

Lissu amesema hayo wakati alipokutana na watanzania wanaoishi Virginia, Maryland na Washington nchini Marekani Jumamosi jioni.

Katika hotuba yake iliyodumu kwa takriban muda wa saa nne ambapo kulikuwa na kipindi cha maswali na majibu ameeleza kuwa ni wajibu wa watanzania kuwashinikiza wauaji kuwajibika.

“Lazima tuseme, kama husemi tukubaliane serikali inapouwa ni sawasawa,” ameeleza umati wa Watanzania waliokutana jijini Washington.

Lissu amewakumbusha Watanzania waliojitokeza kwa wingi katika mkutano huo kuwa Tanzania mwaka 1966 tayari ilikuwa imesaini mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu na kuwa hakuna mkataba wa haki za binadamu ambao hatujausaini.

Wajibu wa Tanzania kwa dunia

“Sisi taifa la Tanzania tunawajibu kwa dunia, [We have obligations to the world]. Tulipopata uhuru Katiba yetu ya mwaka 1961 inasema tutafuata haki za binadamu kama zilivyo andikwa kwenye tangazo la haki za binadamu za Dunia [as numerated in the Universal Declaration of Humanrights],” Kiongozi huyo amesisitiza.

“Hiyo mikataba tuliosaini ni wajibu wetu kwa dunia, tumewaambia dunia kwamba hatutauwa watu wetu,” ameongeza.

Lissu ameeleza kuwa wale ambao wanasema arudi sasa Tanzania, wasubiri kwanza kwani kuna kazi ya kufanya.

“Kuna jukumu la kuwaambia dunia kuwa serikali yetu imeacha kutekeleza jukumu lake la kimataifa. Lakini hatuwezi kusema Tanzania, kwa sababu ukisemea huko utapotezwa,” amesema mwanasiasa huyo.

XS
SM
MD
LG