Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:15

Lissu aelezea ukiukwaji wa haki za binadamu Tanzania


Tundu Lissu
Tundu Lissu

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) nchini Tanzania, Tundu Lissu ametoa waraka wa kwanza na kuuita “Barua Kutoka Kitanda cha Hospitali ya Nairobi” akiahidi kuendelea kuandika nyingine kadiri atavyopata fursa.

Mbunge huyo, ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mnadhimu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, anaendelea na matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi Septemba 7 akiwa nje ya makazi yake Area D mjini Dodoma akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge saa 7:00 mchana.

Katika waraka huo alioutoa Alhamisi, Lissu amezungumzia ukiukwaji wa haki za binadamu na amegusia onyo la serikali kwa viongozi wa dini akisema linakiuka uhuru wa kutoa maoni.

Rais huyo wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), pia amedokeza suala la watu kutekwa akimtaja mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda ambaye leo anatimiza siku 40 tangu alipotekwa na watu wasiojulikana eneo la Kibiti mkoani Pwani alipokuwa anafanyia kazi.

“Watanzania ambao wamekuwa wakitumia uhuru wao wa maoni kutoa mawazo wamekuwa wakikamatwa na kushtakiwa mahakamani... mwanachama wa Chadema, Ben Saanane na mwandishi wa Mwananchi (Azory Gwanda) wametoweka na hawajulikani walipo. Hakuna uchunguzi au taarifa za kutoweka kwao uliotangazwa,” amesema.

Lissu ambaye pia ni mwanasheria wa Chadema amesema vyombo vya habari vimekuwa katika wakati mgumu baada ya kukutana na mkono wa sheria, ikiwamo kufungiwa pale vinapoandika habari zinazotafsiriwa kuwa ni za kichochezi au uongo.

Akizungumzia mambo yaliyojitokeza na yanayoendelea katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano, Lissu alisema kumekuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora, huku viongozi wa upinzani na wanaharakati wakikamatwa na kuwekwa mahabusu.

Amevilaumu vyombo vya dola akisema tangu aliponusurika kuuawa akiwa eneo lenye ulinzi, mpaka sasa hakuna mtuhumiwa hata mmoja anayeshikiliwa kuhusika na tukio hilo.

Kuhusu onyo la Serikali kwa viongozi wa dini kuzungumzia siasa lililotolewa juzi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Lissu amesema ni mwendelezo wa kuwazuia watu wasitumie uhuru wao kuzungumza na kukosoa wanapoona mapungufu katika serikali au watendaji wake.

XS
SM
MD
LG