Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:57

Marekani : Balozi Masilingi akanusha tuhuma za Lissu dhidi ya serikali


Mahojiano maalum : Mkuu wa idhaa ya Kiswahili VOA Mwamoyo Hamza (Kulia) akiwahoji Kiongozi wa Upinzani Tundu Lissu (wapili kutoka kushoto) na Balozi wa Tanzania, Marekani Wilson Masilingi Jumatano Februari 6, 2019.
Mahojiano maalum : Mkuu wa idhaa ya Kiswahili VOA Mwamoyo Hamza (Kulia) akiwahoji Kiongozi wa Upinzani Tundu Lissu (wapili kutoka kushoto) na Balozi wa Tanzania, Marekani Wilson Masilingi Jumatano Februari 6, 2019.

Mnadhimu wa kambi ya Upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema kuwa ni hoja ya kijinga inayotolewa na serikali kuwa yeye anazuia uchunguzi kufanyika baada ya shambulizi la risasi lililofanywa na watu wasiojulikana dhidi yake na dereva wake nchini Tanzania.

“Samahani sana kwa lugha yangu, hii ni hoja ya kijinga sana,” alijibu Tundu Lissu wakati wa mahojiano maalum yaliyofanywa na Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili VOA, Mwamoyo Hamza. Balozi wa Tanzania nchini Marekani Wilson Masilingi pia alishiriki katika mahojiano hayo Jumatano, Washington, DC.

“Kama ningelikufa na dereva wangu angelikufa kusingekuwa na uchunguzi?” alihoji Lissu.

Madai ya kutotoa ushirikiano

Kwa upande wake serikali ya Tanzania imekuwa ikiendelea kudai kuwa Tundu Lissu amekuwa hatoi ushirikiano na hivyo kuchelewesha kukamilika kwa uchunguzi huo. Naye Lissu amekuwa akilalamika kuwa shambulizi alilofanyiwa mpaka hivi sasa halijapata ufumbuzi wa kiuchunguzi.

Tundu Lissu akiwa kwenye matibabu baada ya kupigwa risasi
Tundu Lissu akiwa kwenye matibabu baada ya kupigwa risasi

Akijibu shutuma zilizotolewa na Lissu, Balozi wa Tanzania, Marekani amekosoa lugha anayotumia Lissu na kusema kuwa anasikitishwa na kitendo chake cha kutotambua kwake kazi nzuri ya serikali.

“Kutotambua kazi nzuri ya serikali ukazunguka dunia nzima unamtukana rais wako, vyombo vya dola, na kuwaambia watanzania kwamba hamna haki nchini kwenu sio sawa,” amesema Balozi huyo.

Tazama mahojiano kamili hapa:

Athari ya ziara ya Lissu

“Kitendo cha Lissu kuzunguka dunia nzima hakisaidii. BBC, Radio Ujerumani -DW, Sauti ya Amerika -VOA, sio mahakama. Unachofanya ni kutuchafua na kutuvunjia heshima na kujichafua yeye mwenyewe.”

Lissu alipoulizwa dhana hasi juu ya kutembea kwake nchi za nje akieleza hali ya taifa la Tanzania na vitendo vya mashambulizi alivyofanyiwa kuwa ni kitendo cha kulichafuwa taifa au yeye kuwa ni adui wa Tanzania, alieleza:

“Lazima tutafautishe kati ya serikali na taifa. Serikali ya Magufuli sio taifa. Serikali inatakiwa kuongozwa na katiba, na katiba yetu imeweka wazi mipaka ya mamlaka. Sisi raia ambao ndio taifa tunahaki ya kuwakosoa viongozi wetu, tunahaki ya kuwaondoa madarakani ikibidi,” ameeleza.

“Kwa hivyo tunapoeleza juu ya matendo mabaya iwe tuko ndani ya Tanzania, au nje ya Tanzania au mahali popote tunatimiza wajibu wetu kama raia,” amesisitiza Lissu.

Rais John Magufuli
Rais John Magufuli

Rais ni nembo ya taifa?

Akijibu hoja ya Lissu, Balozi amesahihisha kwa kusema kuwa nafasi ya rais na amiri jeshi mkuu wa nchi, ni nembo ya taifa na hivyo (raia) hutakiwi kumtukana rais.

“Unazungumza vitu ambavyo havipo na unapaswa uniheshimu kwa sababu mimi ni kaka yako,” Balozi alimnasihi Lissu.

“Mimi kama Balozi nimekuja hapa kutetea heshima ya Tanzania, kwa kuwa wewe umekuwa ukitukana nchi yako,” amesisitiza.

Tanzania inamihimili kamili

Balozi amemkumbusha Lissu kuwa kama kuna sababu zozote za kiushahidi, Tanzania ina Katiba ,inasheria, inamahakama huru na inabunge.

“Huyu hajaenda bungeni kupeleka motion au kupeleka mashtaka mahakamani dhidi ya rais,” amemkosoa.

Je, upinzani ni maadui?

Balozi aliulizwa iwapo upinzani wanaonekana kama maadui wa taifa, kwa vile dunia imekuwa ikishuhudia wabunge wa upinzani wakiwekwa ndani, akiwemo Mbowe, Lema, Sugu, Mdee, Lissu na Zitto.

“Wapinzani si wako bungeni. Kwani hawa ndio wapinzani peke yao. Wapinzani wanakamatwa wanapelekwa polisi, polisi wanawapeleka mahakamani,” alifafanua balozi.

“Na nyinyi mnapaswa kuwakumbusha wapinzani kuwa ukiwa mpinzani hauko juu ya sheria, wewe huwezi kuwa kiongozi wa upinzani au mbunge ukavunja sheria.

Viongozi wa Upinzani wakifikishwa mahakamani
Viongozi wa Upinzani wakifikishwa mahakamani

"Upinzani wako rumande hawajafungwa"

Balozi Masilingi amesema kibaya ni kufungwa bila ya kuwa na hatia, hakuna aliyefungwa, watu wako rumande wanachunguzwa, watapewa haki za kikatiba za kujitetea.

Lissu akijibu madai ya kuwa mpaka hivi sasa baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi hajatumia nafasi yake kuwaomba wabunge wenzake wapeleke muswada bungeni kuanzisha uchunguzi rasmi wa shambulizi hilo, alieleza:

“Siku ambayo nilishambuliwa Septemba 7, 2017, Spika wa Bunge la Tanzania aliamuru kamati ya ulinzi na usalama ya Bunge kuchunguza shambulio dhidi yangu, kamati ilipomaliza uchunguzi ikatengewa tarehe ya kutoa ripoti… ilipofika siku ya kutoa ripoti ikawekwa katika orodha ya shughuli za bunge. Baadae kidogo ikaondolewa.”

"Ripoti ya bunge imezimwa"

Lissu ameongeza kuwa ripoti ya uchunguzi huo haijatolewa mpaka leo. Kwa hivyo sio kwamba uchunguzi haukufanyika, umefanyika lakini umezimwa. Watu ambao hawajachunguza shambulizi hili ni Jeshi la Polisi.

“Jeshi la Polisi la nchi yangu halijahoji mtu yoyote, sio majirani zangu, sio mimi mwenyewe, walisema watakuja Nairobi hawakuja,” ameeleza Lissu.

Balozi amekanusha madai ya Lissu akisema kuwa yeye kama mwakilishi wa serikali ya Tanzania, anataarifa polisi wanaendelea na uchunguzi.

“Mimi nakwambia polisi bado wanachunguza, yeye (Lissu ) anasema hawachunguzi,” amesema.

IGP SIRRO
IGP SIRRO

Lissu auliza serikali ilimhoji nani?

Lissu alisisitiza kuwa serikali ieleze wamemhoji nani, wanatakiwa waweke ripoti hadharani.

“Mbunge amepigwa risasi katikati ya vipindi vya bunge, polisi hawajatoa ripoti hata kidogo,” amesema Lissu.

Hata hivyo Balozi amemkosoa Lissu akisema: Kwa sababu wewe ulikuwa hospitalini mwaka na nusu unaletewa taarifa za kukuchonganisha na serikali na unazikubali kama zilivyo. “Wewe kama mwanasheria huwezi ukachukua ushahidi wa kuambiwa.

Balozi alimuomba Lissu: Kwa nini hutaki kurudi nyumbani ukatoa statement wewe na dereva wako, tukafikia hatma ya uchunguzi.

XS
SM
MD
LG