Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 05:46

Chadema yatoa ufafanuzi juu ya kuondoshwa dereva wa Lissu Tanzania


Freeman Mbowe
Freeman Mbowe

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania kimesema kuondoshwa kwa dereva wa Tundu Lissu nchini baada ya shambulio la kikatili la risasi dhidi yao ni kwa ajili ya usalama wake na kupatiwa matibabu.

Lissu na dereva wake, Simon Mohamed Bakari siku ya Alhamisi, 7 Septemba 2017, mjini Dodoma walinusurika kuuawa kufuatia shambulizi la risasi na wote wawili walihamishiwa katika JIji la Nairobi siku hiyo hiyo usiku kwa ajili ya matibabu na usalama wao.

Ufafanuzi huu umetolewa kufuatia tamko la Jeshi la Polisi nchini Tanzania likimtaka dereva wa Lissu, ambaye walimtaja kwa jina moja Adam kuripoti kwa mahojiano polisi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, SACP, Giless Muroto alisema Jumamosi iliyopita kitendo cha kutoweka kwa dereva huyo na kujificha ni kosa la jinai na kama kuna mtu au watu wanaomficha, wanatenda kosa la jinai, wamfikishe Polisi mara moja bila kukosa kwa kuwa ni shahidi muhimu katika upelelezi.

“Popote alipo dereva wa Lissu, Adam ajitokeze na afike Polisi Dodoma au Makao Makuu ya upelelezi Dar es Salaam ili kutoa maelezo kuhusiana na tukio kwani ndiye alikuwa pamoja na majeruhi,” limesema jeshi hilo.

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe amesema dereva wa Lissu, ambaye yuko pamoja na uongozi wa Chadema Nairobi kutokana na mshituko mkubwa ameendelea kupata matibabu ya kisaikolojia.

Mshituko huo umetokana na kuwa alishuhudia shambulio hilo la kinyama na aliokoka kimiujiza, ameeleza.

Kwa mujibu wa madaktari, dereva huyo anasumbuliwa na msongo mkubwa wa mawazo.

“Kwa hivyo hatukuona busara kuendelea kumwacha nchini hadi hapo hali yake ya kiafya na kiusalama itakapo hakikishwa,” amesema Mbowe.

Mwenyekiti ameongeza kuwa ni dhahiri kwa aina ya shambulio lilivyokuwa, wauaji walikusudia kuwauwa wote, Lissu na Dereva wake.

Taarifa ya Chadema imesema kuwa Lissu anaendelea vizuri na matibabu nchini Kenya.

Wageni mbali mbali mashuhuri kutoka nchini Tanzania, Afrika Mashariki na hata Jumuia za kimataifa wamekuwa wakifanya juhudi kubwa kumtembelea Lissu, taarifa hiyo imeeleza..

Hata hivyo, ulinzi umeimarishwa katika eneo anakotibiwa Lissu na hairuhusiwi wageni kumwona hadi hapo madaktari wakiridhika kuwa hali yake ya kimatibabu inaruhusu.

XS
SM
MD
LG