Baadhi ya maswali yaliyoibuliwa ni pamoja na vipi serikali ilijua gari ambalo Lissu alisema lilimfuatilia akiwa Dar halijawahi kufika Dar es Salaam, ili hali nchi haina kamera barabarani wala kwenye mitaa.
Pia kimehoji ni kwa namna gani Waziri wa Mambo ya Ndani anasema magari yanayofanana na lililokuwa limebeba watu waliomshambulia Lissu yamekamatwa 10, huku kukiwa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusika na shambulio hilo.
“Nahisi labda waziri hakumsikia Lissu Agosti 18 alipofanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa kuna watu wanaomfuatilia na kwamba akiwa maeneo ya Protea Hoteli, aliwaona wakiwa na gari namba T 460 ACV na kuwaambia waache kumfuatilia kila anapokwenda,’’alieleza Alhamisi Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa John Mrema
Kuhusu hatua za upepelezi na kufanikiwa kukamata magari 10,Mrema alihoji magari hayo yanashikiliwaje bila kuwa na watu wanaoyamiliki ama kuyaendesha.
“Yalikuwa yakijiendesha yenyewe? Kama yalikuwa na watu je watu hao wanashiliwa mpaka sasa?,” alihoji.
Alisema ni mkanganyiko kama aliouibua Mwigulu Nchemba, ndio unaofanya Chadema itake suala hilo lichunguzwe na vyombo vya nje ya nchi.
Baada ya tukio la kupigwa risasi Lissu serikali ya Tanzania imesema kuwa gari ambalo Lissu alidai lilikuwa likimfuatilia akiwa Dar es Salaam, lipo Arusha na halijawahi kufika Dar es Saalam.
Kadhalika imesema kuwa katika upelelezi wa sakata la Lissu, hadi sasa magari 10 yanayofanana na linalodaiwa kubeba watu waliomshambulia Lissu yamekamatwa na Jeshi la Polisi.
Akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba amesema gari dogo ambalo Lissu alisema limekuwa likimfuatilia katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, liko Arusha na halijawahi kufanya mizunguko ya aina yoyote jijini Dar es Salaam.
“Utoaji wa taarifa na wenyewe haukuwa rasmi, kwa mfano Lissu aliposema kuna gari inamfuatilia, nilielekeza polisi wakaifuatilia, ikakutwa Arusha kuna gari ndogo ya namba hizo, kwa hiyo kuna moja iliweka namba batili.
Serikali imemtaka Mbunge wa Singida Tundu Lissu kusaidia uchunguzi katika tukio la kushambuliwa na risasi na kujeruhiwa akiwa katika shughuli za bunge mkoani Dodoma, Tanzania.
“Watu wasiojulikana nawatafutia dawa ili wajulikane, hata wanapokimbilia sehemu zisizojulikana na suala la Lissu lipo ofisini kwangu naendelea kulifanyia kazi,” Waziri wa Mambo ya Ndani amesema.
Mwigulu Nchemba ameongeza kuwa: “Sisi kama taifa tunatambua nchi yetu iko kwenye vita ya kiuchumi, sidhani kama kuna wengine wanaweza kuturudisha nyuma, ni vizuri tukashirishana ili kutatua hilo.”