Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:30

Tundu Lissu afafanua shambulizi la kutaka kumuua Tanzania


Tundu Lissu
Tundu Lissu

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu wa chama cha Chadema amedai kuwa kuna viashiria vyote kwamba waliomshambulia kwa risasi akiwa kazini mjini Dodoma, Tanzania, wana uhusiano na serikali.

Lissu alitoa madai hayo katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari Ijumaa mjini Nairobi, Kenya, ambako amekuwa hospitali tangu shambulizi hilo la Septemba 7 mwaka jana.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA aliyehudhuria mkutano huo ameripoti kuwa mbunge huyo wa Singida Mashariki ameitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati suala hili ili ufanyike uchunguzi wa kina wa tukio la kushambuliwa kwake.

Mwanasiasa huyo alirudia madai ya kuishutumu serikali ya Tanzania kwa kuhusika katika shambulizi hilo ambalo mpaka sasa uchunguzi wake unaelekea umekwama.

“Mimi siyo mfanyabiashara utasema nimemdhulumu mtu pesa zake, na huwa sipigani baa, ila tangu mwaka 2010 na hata kabla ya hapo katika historia yote ya bunge la Tanzania na katika historia yote ya kisiasa Tanzania haijawahi kutokea,” amesema Lissu akiwa nchini Kenya.

Lissu alisema kuwa haamini kwamba polisi nchini Tanzania wanachunguza shambulizi hilo kwa sababu si yeye mwenyewe wala dereva wake aliyekuwa naye wakati wakishambuliwa amewahi kuhojiwa na maafisa wa polisi.

Amesema kuwa alipigwa risasi 16 nyingi kati ya hizo zilivunja viungo vyake zikapita, zilizokuwa zimebakia katika mwili wake ni 8, ambapo saba zilitolewa na moja imebakia.

“Wataalam wanasema risasi hiyo iliyobakia mwilini haina madhara na kutakuwa na madhara zaidi wakijaribu kuitoa,” amefafanua.

Lakini mbunge huyo amesema mpaka sasa amepata nafuu kubwa na kwamba kuna mipango ya kumpeleka nje ya Kenya, huenda katika nchi ya Ulaya, kwa matibabu zaidi.

Lissu alimlaumu Rais John Magufuli moja kwa moja kwa sababu hajawahi kuzungumzia tukio la kushambuliwa kwake, ingawa aliandika ujumbe kwenye Twitter na pia kumtuma makamu wake Samia Suluhu Hassan kumtembelea Lissu hospitali.

Akizungumzia zaidi uchunguzi wa shambulizi hilo Lissu amesema mazingira ya shambulizi hilo yako wazi kiasi kwamba hadi sasa kungekuwa kumepatikana maendeleo ya kujua nani waliohusika.

“Nyumba ninayokaa ni sehemu ya nyumba za serikali ambayo nilipangishiwa na Bunge kwa kuwa mimi ni mbunge na pia ni mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani bungeni.”

“Nyumba hizo za serikali huwa zinalindwa masaa 24 lakini siku hiyo nyumba zote ikiwemo ya naibu spika ambye ni jirani yangu haikuwa na askari polisi, lakini siku hiyo kulikuwa hakuna mlinzi yoyote.,” alisisitiza.

Akizungumzia hali ya siasa za Tanzania kwa jumla kiongozi huyo wa upinzania alisema :"Tanzania imebadilika kuwa taifa ambalo hakuna mtu aliye salama. Mawakili wanaweza kurushiwa mabomu kwa kuwawakilisha wateja wao. Nchi ambayo ofisi za mawakili zinaweza kuvamiwa, na mawakili kufungwa jela."

Alisema pia Tanzania kuna ukandamizaji wa vyama vya upinzani nchini na nafasi nyingine za kisiasa. Alilaumu pia vyombo vya habari kwa kutotumia nafasi yao kuchunguza au kuripoti hali halisi ya siasa nchini Tanzania chini ya serikali ya Rais Magufuli.

XS
SM
MD
LG