Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 06:46

Spika akiri kuwepo uvunjifu wa amani nchini Tanzania


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai amekiri kuwepo hali ya uvunjifu wa amani nchini na kuwataka wabunge wachukue tahadhari.

Sambamba na kumuombea mwenzao Tundu Lissu ambaye alishambuliwa kwa risasi akiwa kwenye gari nje ya nyumba yake Alhamisi iliyopita mjini Dodoma, Spika aliwatahadharisha wabunge kuhusu usalama wao.

Ndugai amewataka wabunge kuendelea kumuombea Lissu na wale watakaopata nafasi ya kwenda kumuona jijini Nairobi wampelekee ujumbe.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kuahirishwa kwa Bunge Ijumaa, Ndugai aliwataka wabunge kuwa makini popote wanapokwenda kutokana na kuwapo kwa matukio mengi ya uhalifu nchini.

Aliwataka wasikae sana katika baa, “Yaani tuchukue hatua tu katika maisha yetu kama mnavyosikia matukio ni mengi katika nchi yetu. Usalama unaanza na wewe mwenyewe kwanza.”

“Kwa wale tuliozoea saa 7 usiku tunarudi nyumbani basi tuanze kurudi mapema kidogo. Lakini pia tuangalie usalama wa familia zetu na tuwaambie wapigakura, naona siku hizi watoto wanapotea, watoto wanauawa,” alisema.

Aliwataka wabunge kuwapelekea huo ujumbe wananchi kuwa wawe makini na watoto wao wakati wa kwenda shule na maeneo mengine kwa kuhakikisha wanajua mtu anayewapeleka na kuwachukua.

“Hayo mambo yanayofanana na hayo. Ushauri ni wa ujumla tu,” alisema.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameonya kuhusu uhalifu Katika hotuba yake ya kuliahirisha Bunge.

Majaliwa alisema Serikali haitafumbia macho matukio ya uhalifu na tayari vyombo vya dola vimeagizwa kuhakikisha vinawatafuta kwa mbinu zote, wale wote wanaohusika katika vitendo hivyo.

Alisema Serikali inalaani vitendo vya kupigwa risasi kwa Lissu na Meja Jenerali mstaafu Vincent Mritaba ambaye alishambuliwa kwa risasi Jumatatu iliyopita wakati akiingia nyumbani kwake Ununio jijini Dar ea Salaam.

“Ni mwezi na nusu sasa kuanza kwa utulivu kufuatia vifo vya raia na askari wa jeshi la polisi waliouawa kikatili huko maeneo ya Mbagala – Dar es Salaam, Mkuranga, Rufiji na Kibiti mkoani Pwani.

Nirejee kuwasihi wabunge na Watanzania wote wavute subira wakati Serikali na vyombo vya dola vinashughulikia haya kwa umakini mkubwa,” alisema.

Alisema jambo la msingi ni kila mmoja kudumisha hali ya ulinzi na usalama nchini.

XS
SM
MD
LG