Juhudi za madaktari Dodoma
“Pamoja na juhudi za madaktari za kuokoa maisha yake Lissu lakini ni Mungu ndiye pekee anaweza kupanga hatma ya mtu kuondoka duniani,” amesema Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe Ijumaa.
Mwenyekiti amesema ingekuwa watu hawakuchangia damu Lissu asingekuwa leo katika hali hii. Pia dereva wake anapata matibabu ya kisaikolojia huko nchini Kenya.
“Lissu ameponywa sio kwa juhudi zetu, bali na damu iliyochangiwa na watu asiyowajua na kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu,” amesisitiza Mbowe.
Zoezi la kuchangia damu
Amesema damu hiyo ilichangiwa sio na watu wa Chadema lakini ni watu wa makabila, mataifa na dini mbali pande zote mbili Tanzania na Kenya.
“Japo mambo haya ni siri ya mgonjwa Lissu alipoteza damu nyingi sana, na hivi leo asilimia 95 ya damu anayotumia ni ile aliyochangiwa na hivyo kupona kwake ni miujiza kwa madaktari na watanzania,” Mbowe amefafanua.
Watu waliokuwa wanakwenda kuchangia damu polisi wanadai kuwa walikuwa wanapanga uhalifu kwa nini wamevaa fulana za Chadema, amesema.
Kuzuiwa watu kufanya maombi
Ameongeza kuwa watu wanazuiwa kufanya maombi, polisi inawatawanya kwa nguvu badala ya kutoa ulinzi ili wafanye ibada zao.
“Ile idadi ya askari iliyokwenda kuwazuia wananchi kufanya ibada ingeweza kutumika kuwalinda na wakafanya maombi yao na kuondoka kwa salama," amesema mwenyekiti.
Mbowe amesema kuwa mambo haya "yametuumiza sana Watanzania na limetudhalilisha sana. Kwa wale tunaowasiliana na watu wa mataifa mengine dunia nzima inatushangaa."
Kauli ya serikali
Kufuatia maelezo ya Spika wa Bunge na Mwenyekiti wa kambi ya Upinzani Bungeni, maoni mengi yametolewa na wachambuzi mbalimbali juu ya hatima ya matibabu ya Tundu Lissu baada ya kushambuliwa kwa risasi katika eneo ambalo linaulinzi mkali kwa sababu ni makazi ya viongozi wa ngazi ya juu, wakiwemo mawaziri, na wabunge.
Kauli ya Serikali kwamba iko tayari kugharimia matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu popote pale, imeibua mjadala mzito huku baadhi ya wasomi wakidai ni ya kujikosha baada ya kushindwa kuwajibika tangu kiongozi huyo aliposhambuliwa.
Wasemavyo wasomi na wachambuzi
Wachambuzi Wamehoji ni kwa nini Serikali kuibuka sasa wakati ilipaswa kuwajibika tangu awali kwa kuwa mbunge huyo alikumbwa na tukio la dharura ambalo lilipaswa kushughulikiwa kwa haraka.
“Sijui mantiki yake ni nini...tunashangaa wakati wote huo ilikuwa wapi na sijui huo uamuzi waliochukua ni wa dhati au inaona haya mbele ya jamii,” alisema Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha.
Gazeti la kila siku nchini Tanzania ambalo limemhoji mwanawazuoni huyu, limeandika kuwa amesema kwa namna yoyote ile, kulikuwa hakuna haja ya kusubiri kufuata taratibu ili kufanikisha matibabu ya Lissu kwani jambo hilo lilipaswa kupewa kipaumbele ili kuokoa maisha yake kwanza.
Isemavyo mitandao ya jamii
Watu wengi wameandika katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa kitendo cha kumuondosha Lissu Tanzania kilikuwa ni mwafaka kutokana na shambulizi hilo la risasi za moto ambalo lilimjeruhi vibaya sana.
Mwengine aliyetoa maoni yake kwa vyombo vya habari ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt Richard Mbunda ambaye ameonyesha kupigwa na butaa na kitendo cha Serikali kuchelewa kuwajibika kwa haraka katika tukio la Lissu.
Ameeleza kuwa maelezo yaliyotolewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusu matibabu ya mbunge huyo yalizidi kuchanganya zaidi badala ya kutoa mwanga uliotarajiwa.
Katika maelezo yake kuhusu utaratibu wa matibabu ya wabunge, Spika Ndugai alisema anapaswa kupelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbuli na hali yake ikizidi kuwa mbaya anapelekwa Hospitali ya Apollo, India na si vinginevyo.
Spika Ndugai atoa maelezo
Spika Ndugai alilazimika kutoa maelezo hayo baada ya uongozi wa Chadema kukataa Lissu kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, ikidai kwamba ni kwa kuhofia usalama wake.
Dkt Mbunda ameweka wazi kuwa Lissu alikuwa katika hali tete na kwa maana hiyo hatua zilizopaswa kuchukuliwa ni kuangalia njia zinazoweza kusaidia kuokoa maisha yake na siyo kuweka msaada wenye masharti.
“Serikali ilipaswa kulishughulikia vyema suala hili tena hasa kwa kuzingatia kuwa mwenyewe Lissu amekuwa akiituhumu kuwa inamfuatilia, sasa ingechukua fursa hii haraka ili kujisafisha,” alisema.
Lissu si mwanasiasa tu bali ni kiongozi wa kitaifa
Dokta alisema Lissu licha ya kuwa mwanasiasa mashuhuri lakini pia ni mbunge na kiongozi ndani ya Bunge, hivyo kwa namna yoyote ile Serikali ilikuwa na wajibu wa kuchukua hatua za kuokoa maisha yake kwa kukubaliana na hoja za familia na chama chake.
Ameendelea kusema : “Hakuna gharama inayofanana na uhai wa mtu... hakuna kabisa. Huyu mtu kashambuliwa tena kwa kupigwa risasi nyingi unataka nini kifanyike zaidi ya kwanza kuchukua hatua za haraka kunusuru maisha yake?”
Ushauri wa Profesa Abdul Sherrif
Kwa upande wake Profesa Abdul Sherrif alishangaa kuona suala la matibabu ya Lissu kugubikwa na hisia za kisiasa.
“Huyu ni binadamu anapaswa kwanza kuangaliwa afya yake, lakini watu badala ya kushughulikia matibabu yake wanaingiza mambo ya siasa... siyo jambo nzuri hata kidogo,” alisema.
“Hili suala watu wanaliendesha vibaya kabisa wala hawaangalii tena haki za binadamu wanalibeba kisiasa zaidi,” gazeti hilo lilimnukuu Profesa.