Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 06:23

Chadema yaeleza sababu za kuomba msaada wa FBI, GBI, Scotland Yard


Jaji Mkuu Ibrahim
Jaji Mkuu Ibrahim

Uongozi wa Chadema umeomba uchunguzi wa shambulizi alilofanyiwa Mbunge wa Mkoa wa Singida Tundu Lissu ufanywe na chombo chochote cha uchunguzi huru kama vile FBI (Marekani), Scotland Yard (Uingereza), GBI (Ujerumani) ambacho pande zote mbili (serikali na upinzani) unaimani nacho.

“Serikali haitaki, na Alhamisi kwa bahati mbaya sana mheshimiwa Jaji Mkuu akatoka na kauli kwamba vyombo vya ndani havijashindwa kufanya uchunguzi. Sina kusudio la kubishana na Jaji Mkuu, lakini kama kiongozi muandamizi wa Chadema nadiriki kusema kitu kimoja, mshukiwa wetu namba moja kwenye shambulio la Lissu ni vyombo vya ulinzi na usalama,” amefafanua, Mwenyekiti wa Chadema, Mbunge wa Jimbo la Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Freeman Mbowe.

Lakini Mwenyekiti huyo amesema ni vigumu sana kusema ni tukio la kijambazi, hakuna ujambazi pale.

“Hilo nalisema bila ya kumumunya maneno. Viashiria vyote vya tukio lile la kushambuliwa Lissu tangu linatokea, kauli za viongozi, kusita kwa viongozi, na baadae kauli za kujiosha, na mazuio yasiokuwa na mantiki, kwa mtu yoyote mwenye akili timamu atasema mshukiwa namba 1 ni vyombo vya ulinzi na usalama. Ukiniuliza ni nani, katika vyombo vya ulinzi na usalama, simjui mimi,” amefafanua Mbowe.

Mapema Alhamisi Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma alisema wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu mkutano wa majaji na mahakimu wa Jumuiya ya Madola unaofanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania kuanzia Septemba 24 hadi Septemba 28 kwamba : “Nadhani tumekubaliana, hili ni tukio la kihalifu, uhalifu mkubwa sio mdogo, ni jaribio la kuua.

Jaji Mkuu akaongeza kuwa kitu cha kwanza ni kukusanya ushahidi na huo ushahidi utakusanywa hapa hapa Tanzania, "asikudanganye kwamba mtu kutoka nje atakuwa na uwezo wa kukusanya ushahidi. Ushahidi unakusanywa Tanzania."

Mwenyekiti Mbowe amesistiza kuwa hadi “sisi kudai vyombo huru vya kiuchunguzi ni kutokana na madhila mbalimbali ambayo tumeyapata kwa muda mrefu na tukaona vyombo vya ndani vya ulinzi na usalama havina msaada wowote.”

Baada ya uchaguzi wa 2015 Mwenyekiti wetu wa mkoa wa Geita Alphonce Mawazo aliyekuwa pia mgombea wa ubunge alishambuliwa mchana kweupe na watu ambao wanajulikana, “wenzetu wanatwambia kwamba watu hawa hawajulikani, wakati waliomshambulia Mawazo wanajulikana,” amesisitiza Mbowe.

Mbowe amesema polisi hawakuchukua hatua yoyote walisema wanachunguza, lakini hawakuchunguza, “Mawazo mwaka wa pili unapita inamaana yamesahaulika.”

Mwengine amemtaja kuwa ni Ben Saanane ambaye alikuwa msaidizi wake na amepotea huu ni mwaka wa pili unakwenda; “tumepiga kelele ndani ya bunge na nje ya bunge na kupitia vyombo vya habari, hakuna hatua zinazochukuliwa.”

Mbowe amesema: “Binafsi nilimuuliza Waziri Mkuu swali kwa nini serikali isiruhusu vyombo vya upelelezi vya nje kama Scotland Yard ambao wanautaalamu mkubwa wa forensic investigation”, wale hawawezi kuja bila ya serikali ya Tanzania kutoa maombi.”

“Na hata sasa hivi tumezungumza na vyombo vya Marekani, Uingereza, Ujerumani wako tayari kutoa msaada lakini baada ya kupata maombi kutoka serikali ya Tanzania,” amesema.

"Kama serikali inajiamini ruhusuni hawa watu waje wafanye uchunguzi watoe ushahidi, watu wenye utaalamu wao waje waweke vielelezo hapa, huo ndio msimamo wa Chadema.

Sasa CJ tunaomba yeye asubiri mambo yaje mahakamani, mambo ya uchunguzi hayako katika mhimili wake. Mhimili wako ni wa mahakama, hauhusiki katika jambo hili,” Mbowe amesema.

Tunamuomba mheshimiwa tunamuheshimu sana hatutaki kugombana na mhimili wake, ameongeza.

“Tunataka serikali itambue kwamba tunapoomba msaada wa kiuchunguzi ni kwa sababu hatuna imani na vyombo vya usalama. Watu wengi wamepotea, wameuawa, wamepigwa risasi mchana na hakuna hatua ya maana iliyofanyika. Hatuna imani kwamba uchunguzi wa safari hii utakuwa tofauti,” amesisitiza Mbowe.

XS
SM
MD
LG