Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 02:14

Kesi ya Kabendera : Mawakili wasisitiza umuhimu wa upelelezi kukamilika kabla ya mtuhumiwa kushtakiwa


Eric Kabendera
Eric Kabendera

Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mwandishi wa habari za uchunguzi nchini Tanzania , Erick Kabendera, imeahirishwa Jumatatu hadi Agosti 30, 2019 baada ya upande wa serikali kusema haujakamilisha upelelezi na pia hakimu mkazi mwandamizi, Augustine Rwizile, kupata udhuru.

Kabendera anashtakiwa kwa makosa matatu ikiwemo kukwepa kodi kiasi cha Shilingi milioni 173,247,047.02, utakatishaji fedha na kujihusisha na genge la uhalifu, makosa ambayo yote hayana dhamana.

Erick Kabendera alikamatwa nyumbani kwake maeneo ya Mbweni Dar es Salaam, siku ya Julai 29, 2019, na watu waliokuwa hawajajitambulisha. Baada ya habari za kutatanisha kusambaa kwamba ametekwa, polisi walithibitisha kuwa amekamatwa na anahojiwa. Alihojiwa na vyombo kadhaa vya ulinzi na usalama likiwemo Jeshi la Polisi pamoja na Idara ya Uhamiaji.

Mawakili wanaomtetea mwanahabri Kabendera, wakiongozwa na Jebra Kambole, wameiomba Mahakama kuutaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi sababu mtuhumiwa yupo mahabusu hivyo ucheleweshwaji wa upelelezi utasababisha mtuhumiwa kuendelea kukaa mahabusu kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa Mtandao wa kutetea haki za binadamu Tanzania, Onesmo Ole Ngurumo amesisitiza kufanyika kwa upelelezi wa kutosha kwanza kabla watuhumiwa wa kesi kama za uhujumu uchumi kufunguliwa mashataka.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mwandishi Kabendera bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajali ya kutajwa.

Wakati Simon akieleza hayo, wakili wa Kabendera, Jebra Kambole ameutaka upande wa mashtaka kuhakikisha upelelezi wa shauri hilo unakamilika kwa wakati kutokana na mteja wake kutokuwa na dhamana.

"Hatuna pingamizi kuhusu kupata udhuru kwa hakimu, ila tunaomba upande wa mashtaka wajitahidi kukamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi hii iweze kuendelea kwa sababu mteja wangu anaendelea kusota rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana,” amesema Kambole.

Kesi iliyokuwa inatakiwa kusikilizwa Jumatatu ni ya kuomba dhamana, iliyokuwa imewasilishwa mahakamani hapo na mawakili wa Mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG