Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 02:17

Tanzania : Kabendera kushtakiwa kwa kukiuka sheria ya mtandaoni


Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Ki-moon akizungumza na mwandishi wa Tanzania Erick Kabendera.
Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Ki-moon akizungumza na mwandishi wa Tanzania Erick Kabendera.

Mwandishi wa habari za uchunguzi nchini Tanzania, Erick Kabendera, sasa anashikiliwa rasmi kituo cha polisi kati, jijini Dar es Salaam, kwa madai ya kuchapisha habari yenye taarifa za uongo mtandaoni kinyume na sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015.

Vyanzo vya habari vinasema kuwa Kabendera anadaiwa kuandika na kuchapisha habari inayodaiwa kuwa ya uongo yenye kichwa cha habari kinachosomeka kuwa, *Mkosoaji mwingine wa Rais Magufuli anyamazishwa," katika ripoti iliyochapishwa kwenye gazeti la nje la Economist.

Awali mwandishi huyo wa kujitegemea alikamatwa nyumbani kwake Mbweni, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam katika mazingira ya kutatanisha na watu wanaodhaniwa kuwa ni askari kanzu mnamo Julai 29, 2019. Siku moja baadaye polisi ilisema amekamatwa kuulizwa kuhusu uraia wake.

Hata hivyo, kukamatwa kwa Kabendera kuliibua hali ya sintofahamu miongoni mwa wadau wa habari kutokana na mlolongo wa matukio ya watu kutekwa na kupotea nchini katika siku za hivi karibuni, jambo lililofanya taasisi na mashirika ya haki za binadamu nchini ikiwemo Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kutoka hadharani kulaani kitendo hicho na kuomba mamlaka za usalama nchini Tanzania zimwachilie huru mwandishi huyo ikiwa ni kweli zinamshikilia.

Baadae Idara ya Uhamiaji ilijitokeza hadharani na kukiri kumshikilia mwandishi huyo kwa madai ya kutilia shaka uraia wake, ambapo mamlaka hiyo ya serikali ilidai kumwandikia barua ya wito mwandishi huyo kwa ajili ya kumhoji lakini alikaidi, ndipo ilipoamua kumkamata kwa kushirikiana na jeshi la polisi.

Mnamo mwaka 2013 mamlaka ya uhamiaji nchini Tanzania ilishuku uraia wa Kabendera, lakini baadae ilimsafisha kuwa ni raia halali wa Tanzania.

Kwa mujibu wa jopo la mawakili wa Kabendera kutoka THRDC, Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania, imemwachia lakini jeshi la polisi limemkamata tena kwa kukiuka sheria ya makosa ya mtandao kwa kuchapisha maudhui yanayodaiwa kuwa ya uongo.

Jopo la mawakili kutoka THRDC wanaendelea kufuatilia taratibu za dhamana na Watetezi TV itaendelea kukujuza kile kitakachokuwa kinaendelea.

XS
SM
MD
LG