Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:22

Waziri Kabudi akanusha hakusema Azory Gwanda amekufa


Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Palamagamba Kabudi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Palamagamba Kabudi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Palamagamba Kabudi amekanusha kuwa alithibitisha 'kifo' cha mwanahabari Azory Gwanda wakati wa mahojiano yake na Shirika la Habari la Uingereza, BBC.

Msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania, Dkt Hassan Abbas amemnukuu Profesa Kabudi kwa kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter akisema: "Nimepokea kwa masikitiko taarifa potofu zinazoendelea kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii ikinukuu kimakosa mahojiano yangu kwenye kipindi cha Focus on Africa zikidai kuwa nimethibitisha kwamba mwanahabari Azory Gwanda amefariki dunia."

Katika maelezo yake Waziri amesema bado haijulikani kama Gwanda yungali hai: "Mpaka sasa hakuna uthibitisho kuwa Azory yuko hai au amefariki. Vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuchunguza tukio hilo na matukio mengine yaliyotokea katika machafuko ya Kibiti, Pwani yaliyosababisha ama watu kadhaa kupoteza maisha au kupotea."

Maelezo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Palamagamba Kabudi kuwa mwandishi wa habari Azory Gwanda, ambaye alikuwa ametoweka kwa takriban miaka miwili, amefariki imepelekea Kamati ya Kulinda haki za wanahabari duniani (CPJ) kutaka “maelezo kamili kwa umma juu ya kifo” cha mwandishi huyo wa kujitegemea.

Kabudi alitoa maelezo hayo yakushitusha wakati wa mahojiano yake na Shirika la Habari la BBC Jumatano.

Wakitoa hisia zao baada ya taarifa hiyo ya waziri, CPJ imeitaka serikali ya Tanzania “kutoa maelezo kamili kwa umma” juu ya kile kilichomfika Gwanda kupelekea kuuawa.

Katika mahojiano yake katika kipindi cha BBC “Focus on Afrika” Kabudi alisema kuwa Gwanda “alipotea na kufa” nchini Tanzania, mashariki mwa wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani.

Waziri huyo alisema kuwa serikali tangu wakati huo “imeweza kuzuia misimamo mikali” katika mkoa huo.

Gwanda alitoweka Novemba 21, 2017, baada ya kuchunguza mauaji yaliyokuwa yanafanywa kwa siri na kupotea kwa watu katika jamii yake. Serikali ya Tanzania haijaweza kutekeleza ahadi ya uchunguzi wa kupotea kwa mwandishi huyo, imesema CPJ.

Kwa kipindi cha mwaka moja na nusu, familia ya Azory Gwanda na vyombo vya habari vya Tanzania vimekuwa vikiiomba serikali kuelezea kile kilichomtokea mwandani wao na mfanyakazi mwenzao, alisema Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa CPJ Robert Mahoney kutoka New York.

“Ghafla waziri wa mambo ya nje anataja kama jambo la kawaida, kuwa inaelekea mwandishi huyo amekufa. Maelezo haya yote hayatoshelezi na yanasikitisha. Lazima serikali ya Tanzania mara moja iufahamishe umma taarifa zote ilizokuwa nazo juu ya kifo cha Gwanda.”

Kabudi ameiambia BBC kuwa serikali ya Tanzania “haijifaharishi” kwa kutoweka kwa raia na mauaji yaliyotokea Rufiji, ambayo amesema ilisababisha vifo vya maafisa wa polisi na viongozi wa chama tawala cha CCM. Waziri wa mambo ya nje alisema serikali inachukuwa hatua kuhakikisha raia na waandishi wako salama.

Lakini, CPJ imesema utafiti wake juu ya hali hii isiyo ya kawaida inaonyesha “uhuru wa waandishi kuuawa au kutoweka unachangia katika mazingira yanayoshajiisha uvunjifu wa Amani dhidi ya waandishi.”

XS
SM
MD
LG