Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 09:53

Watu 348 wadaiwa kupotea kusini mwa Tanzania


Mbunge Zitto Kabwe
Mbunge Zitto Kabwe

Serikali ya Tanzania imetakiwa kulieleza Bunge kinachoendelea kusini mwa Tanzania, ambapo inadaiwa kuwa hadi sasa zaidi ya watu 348 wamepotea.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt Mwigulu Nchemba, kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo.

Mbunge huyo amedai kuwa kati yao 68 wamethibitika kuwa wamefariki dunia baada ya kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

“Nina orodha ya watu 348 wakazi wa wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji," Zito alisema Ijumaa.

Zitto, ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, alitoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma alipokuwa anachangia mjadala wa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka ujao wa fedha.

Alisema Dkt Nchemba analiomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh. bilioni 945 kwa ajili ya wizara yake na kati yake, Sh. bilioni 596 sawa na asilimia 63 ya bajeti yote inakwenda Jeshi la Polisi ambalo limeshindwa kuchunguza tukio la kupigwa risasi Lissu.

Mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Kusini (Chadema), alisema mlolongo wa matukio ya watu wengi kutekwa na watu wasiojulikana na Jeshi la Polisi kushindwa kutoa maelezo huenda ukaleta shida kubwa ndani ya nchi.

Aliongeza kuwa :“Mbunge Kilwa (Kusini), Ndugu (Suleiman) Bungara amezungumza kwa hisia na wakati mwingine muache watu wazungumze kwa hisia kwani wakati ndiyo huu wanaongea yale ambayo yanawahusu."

“Tarehe 12 Juni, mwaka jana, mama mmoja anaitwa Ziada Salum wa Kitongoji cha Maparani Kibiti, alichukuliwa na Jeshi la Polisi saa sita mchana, na leo ni miezi 11 mama huyo hajaonekana, yupo wapi?" Zitto alihoji.

Mbunge huyo aliendelea kueleza kuwa siku hiyo hiyo, kuna mtu anaitwa Rukia Mhoni na Tatu Mhoni ambao ni ndugu na kwa pamoja walichukuliwa na Jeshi la Jolisi na miezi 11 hawajaonekana.

Alisema wapo watu ambao wana miaka miwili hawajulikani walipo wakiwamo Ben Saanane, Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mwandishi wa habari Azory Gwanda ambaye hivi karibuni mkewe alijifungua mtoto bila uwapo wa huduma za baba wa familia.

“Wakati wa hotuba ya Tamisemi (Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) na Utawala Bora, nilizungumza kuhusu kupotea kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo, Kanguye, ambaye pia ni diwani wa CCM," Zitto alieleza.

Zitto alihoji: "Wiki iliyopita mama mzazi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo, Kanguye alifariki dunia akiwa hajui mwanaye yupo wapi. Tukasema sawa, hii ni serikali moja, Wizara ya Mambo ya Ndani itakuja. Sasa imekuja, haya tuelezeni kama siyo kazi ya Usalama wa Taifa, ni kazi ya polisi. Polisi watueleze ndugu Kanguye yuko wapi."

Zitto pia aliitaka serikali kuhakikisha inatekeleza matakwa ya Katiba ambayo alieleza kuwa katika Ibara ya 15(1) na (2) inaweka wazi kuwa kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru.

XS
SM
MD
LG