Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:18

Waandishi katika mazingira hatarishi Afrika Mashariki


FILE - Waandishi na wanaharakati wakiandamana katika siku ya uhuru wa habari duniania Day, May 3, 2018, in Nakuru, Kenya.
FILE - Waandishi na wanaharakati wakiandamana katika siku ya uhuru wa habari duniania Day, May 3, 2018, in Nakuru, Kenya.

Wakati ulimwengu unaadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Ijumaa, hali ya uhuru wa vyombo hivyo inaendelea kukabiliwa na misukosuko mingi kadri siku zinavyosonga mbele.

Uganda ni miongoni mwa nchi 22 zenye rikodi mbaya ya ukandamizaji wa uhuru wa habari barani Afrika. Ripoti ya Waandishi wa Habari bila mipaka 2019, kuhusu uhuru wa habari duniani inaeleza matukio ya waandishi wa habari kutishiwa na kupigwa ni ya kawaida nchini Uganda, wakati maafisa wa usalama wakiongoza dhuluma hiyo dhidi ya waandishi wa habari.

Pia inasema kuwa mwanahabari yeyote anayeandika habari za kuikosoa serikali, analengwa, kuchapwa, kutekwa nyara na vifaa vyao kuharibiwa.

Rais Yoweri Museveni

Ripoti hiyo inasema kwamba Rais wa Uganda Yoweri Museveni hapendi kukosolewa na mara nyingi ametumia lugha ya madharau dhidi ya waandishi wa habari na hata kuwaita vimelea, yaani watu ambao maisha yao yanategemea wengine.

Maafisa wa vyombo vya usalama, huvamia vituo vya habari, huwapiga waandishi na hata kuvizima, hasa wanapojadili masuala yanayokosoa serikali.

Mamlaka ya mawasiliano Uganda, UCC, wiki hii imeamrisha kusimamishwa kazi wahariri, watangazaji na wasimamizi wa vipindi katika vituo vikuu vya habari 15, baada ya kupeperusha habari juu ya mwanasiasa wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, alipokamatwa na polisi.

Vituo hivyo ni pamoja na NTV, NBS, BBS TV, Capital radio, Akaboozi FM, Runinga inayomilikiwa na serikali, Bukedde TV, miongoni mwa vingine.

“Kwa kiwango hiki, hali si hali tena. Ni dhahiri uandishi wa habari za kisiasa ni kosa la jinai nchini Uganda. Kitendo cha mamlaka ya mawasiliano, UCC, kuwafukuza kazini wahariri, na watangazaji katika vituo vya habari zaidi ya 15, ni ishara uhuru wa uandishi wa habari umetoweka na ni kilele cha vita dhidi ya uandishi wa habari.

“Vyombo vya habari sasa vinazuiliwa kupeperusha matangazo ya moja kwa moja? UCC imetoa wapi mamlaka ya kuagiza waajiri wa waandishi wa habari kuwafukuza kazi? Tunapoelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2021, hakuna matarajio kwamba waandishi wa habari watakuwa salama na kufanya kazi yao kwa uhuru unaohitajika. Hali ni tete,” ameandika kwenye Facebook, Robert Sempala, wa shirika la kutetea haki ya waandishi wa habari Uganda, HRNJ.

Amri ya UCC, inajiri siku chache baada ya wakuu wa wilaya katika wilaya nne, kuzima mitambo ya radio, vituo hivyo vilipokuwa vinamhoji aliyekuwa mgombea wa urais Dkt Kiiza Besigye katika sehemu na siku tofauti.

Rais John Magufuli

Uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania umedorora zaidi tangu kuingia madarakani Rais John Pombe Magufuli mwaka 2015.

Tanzania imeshuka nafasi 25 chini katika jadwali la Ripoti ya Uhuru wa Habari 2019 na imetajwa ni ya 118 barani Afrika, ambapo waandishi wa habari wanaendelea kuzuiliwa kufanya kazi zao kulingana na maadili ya kazi.

Baadhi ya vipindi vimezimwa hasa vinavyoonekana kukosoa serikali au kufanya mahojiano na wanasiasa wa upinzani, wandishi kupigwa hadi kujeruhiwa na hata kutoweka.

Wanaoandika habari kwenye mitandao wamewekewa masharti magumu ikiwemo kutakiwa kulipa dola 900 kwa usajili wa wavuti au blogi, kiasi cha pesa kinachotajwa kuwa kikubwa zaidi kwa lengo la kuwazuia wachapishaji.

Ipo pia sheri inayozuia uchapishaji wa takwimu bila idhini ya serikali. Ving’amuzi vya kampuni huru za kupeperusha matangazo ya runinga ndani ya Tanzania vimezimwa, huku matangazo ya moja kwa moja kutoka bungeni nayo yakipigwa marufuku.

Wachambuzi wanasema waandishi wa habari wa Tanzania sasa wanaogopa kuandika habari za upekuzi na wengi sasa wanaandika kuhusu ziara za wanasiasa wa chama tawala na mipango ya serikali bila kuihoji wala kuikosoa.

Hatma ya Mwandishi Azory Gwanda

Waandishi wa habari wanatishiwa, kukamatwa na hata kutoweka. Mfano ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda aliyetoweka May 21 2017 na hadi sasa hajulikani alipo.

Bungeni, April 23 mwaka 2019, Waziri wa Habari Harrison Mwakyembe, akijibu maswali hukusu wanaouliza alipo Azory Gwanda, wakiwemo wabunge, alisema:

“Tunaongelea kesi ambayo ni dhaifu sana, tena sana. Mwandishi huyu amepotea eneo ambalo mamia ya watanzania wengine wamepotea. Hawaulizwi wao. Huyu mtu mmoja ndio dhahabu. Halafu inaulizwa serikali ambayo yenyewe imeshughulikiwa kiasi kikubwa kwelikweli. Maafisa wetu wa serikali wengi wamekufa kule lakini leo tunaulizwa kuhusu mtu mmoja. Sio haki kabisa. Najua mnawatumikia wazungu na wafadhili wengi, wacha wayapate lakini mimi ninachosema hatujakosa chochote, wacha tushushwe hayo madaraja, sisi tunauthamini uhuru wetu kwanza na hayo madaraja baadaye”.

Gwanda alikuwa akiandika habari za uchunguzi na mauaji katika mji wa Kibiti, kilomita 130 kusini mwa Dar-es-salaam, na tangu kutoweka kwake yapata mwaka mmoja na siku 134 sasa, maafisa wa usalama wa Tanzania wanasema bado wanafanya uchunguzi bila maelezo yoyote kumhusu.

Rais Uhuru Kenyatta

Serikali ya Kenya chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta inaorodeshwa katika nafasi ya 100 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa utafiti katika ripoti ya waandishi wa habari wasio na mipaka ya mwaka 2019, ikiwa imeshuka nafasi nne, kutoka nafasi ya 96 mwaka 2018.

Maafisa wa usalama wametajwa sana katika ripoti hiyo, kwa kuwapiga waandishi wa habari, wakifuatiwa na raia wa kawaida.

Wandishi wanatishiwa na wanasiasa huku wakishambuliwa na wafuasi wa wanasiasa.

Vifaa vya waandishi wa habari vinachukuliwa n ahata kuharibiwa.

Waandishi wa habari wanaoandika habari za kisiasa wanakamatwa na kuzuiliwa huku vituo vya habari vikiwa katika hali ya hatari kuzimwa kwa mda.

Waandishi wanaopiga picha ambazo maafisa wa usalama wanahisi kwamba zinaweka wazi maovu wanayofanya, wanalengwa na maafisa hao, kupokonywa vifaa vyao na picha kufutwa.

Kelvin Ogome ni mwandishi wa habari wa kituo cha KUTV, Nairobi.

“Uhuru wa vyombo vya habari nchini Kenya haupo. Kilichopo ni biashara ya habari kwa sababu habari nyingi zinaegemea upande mmoja wa kisiasa. Wandishi pia wanaogopa kuandika kuhusu baadhi ya mambo yanayowahusu wanasiasa Fulani. Vyombo vingi vy ahabari Kenya vinamilikiwa na wanasiasa kwa hivyo waandishi katika vyombo hivyo hawawezi kuandika habari kwa usawa wakati mwajiri wao ana msimamo tofauti” amesema Ogome

Wellington Nyongesa, mhariri katika kituo cha habari cha KTN, ambaye amefanya kazi ya uandishi wa habari kwa mda mrefu, ana mtazamo kwamba serikali ya Kenya, imebadilisha mbinu za kuwadhulumu waandishi wa habari.

“wanatumia njia za hongo. Kuna vitisho vya namna lakini sio kama zamani ambapo mwandishi wa habari alikuwa hata anapigwa. Visa vya waandishi wa habari kupigwa ni vichache. Serikali pia inaamua kunyima baadhi ya vyombo vya habari matangazo na hivyo kutopata pesa” amesema Nyongesa.

Lakini Nyongesa vile vile anasema uhodari umepungua kati ya waandishi habari.

“sekta ya wanahabari inakosa uhodari. Si kwamba wanazuiwa lakini wanahabari ni waoga. Udhaifu upo katika vyombo vy ahabari vyenyewe. Mimi binafsi hupeperusha Makala yanayoikosoa serikali vikali sana. Nimewahi tu kupigiwa simu na serikali ikilalamika lakini sijawahi kudhulumiwa. Vitisho vipo, lakini kama una ujasiri, sio vitisho vya kukuzuia kufanya kazi yako” ameongeza kusema Nyongesa.

Rais Pierre Nkurunziza

Chini ya uongozi wa Rais Pierre Nkurunziza Burundi nayo imechukua hatua kali dhidi ya waandishi wa habari, na hata kufunga vyombo vya kimataifa ambavyo vinaweza kuandika habari zisizoegemea upande wowote.

Baadhi ya viuto vya habari ndani ya nchi navyo vimefungwa huku kituo kilichokua kikikosoa serikali kikipigwa mabomu na kuharibiwa kabisa.

Waandishi wa habari wanafuatiliwa kwa haribu sana kujua wanayoandika, huku wasimamizi wa vituo wakikosa uhuru wa kutangaza baadhi ya habari.

Matumizi ya mitandao ya kijamii

Kufuatia hali mbaya inayovikumba vyombo vya habari, wananchi sasa wanatafuta habari kwenye mitandao ya kijamii.

Video za moja kwa moja zinawekwa na mtu yeyote kwenye mitandao ili kuwasilisha ujumbe, huku wanaotumia wakitumia majina bandia hasa katika nchi ambapo usambasaji wa habari unabanwa sana, kuweka habari kwenye mitandao na hata kuwakosoa viongozi.

John Baptist Imokola, ni mhariri wa habari na mawasiliano katika chuo kikuu cha Makerere, Uganda.

“siku zote watu watatafuta mbinu mpya za kuishi endapo wanahisi mamlaka inawanyanyasa. Wanapoweka sheria kandamizi kwa vyombo vya habari na mazingira magumu kwa waandishi wa habari, raia wanakimbilia mitandao ya kijamii ambapo picha na habari zinawekwa bila hata kuhaririwa na watu kujua kila kinachoendelea jinsi kilivyo na hivyo kuimarisha uaminifu wa matukio. Mitandao ya kijamii inaimarika sana na kuvutia kila mtu hata hao wanaounda sheria kandamizi” ameeleza Imokola.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu

Matamshi yake Imokola, yanakaribiana na ya Anna Henga, mkurugenzi wa kituo cha sheria nahaki za kibiandamu nchini Tanzania, anayesema kwamba japo viongozi serikalini wameanza kutunga sheria za kubana mitandao ya kijamii, matumizi yake yameongezeka sana.

“zamani ulikuwa unakimbia nyumbani saa mbili kamili kutazama habari kwenye runinga. Kwa sasa, hamna hata habari. Wanajaribu kufunika mambo ambayo kila mtu anayajua. Kidogo vyombo vya habari vya nje vinajitahidi kueleza ukweli lakini hata navyo, vinapata ugumu katika baadhi ya mataifa. Tunatumia sana mitandao ya kijamii sasa hivi”

Na wakati dunia inaadhimisha uhuru wa vyombo vya habari, viongozi serikalini wanaendelea kuunda sheria kudhibiti usambasaji wa habari hata kwa kutumia internet na mitandao ya kijamii.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Kennes Bwire, Sauti ya Amerika, Washington DC

XS
SM
MD
LG