Mjadala huo umeendelea kuwepo katika vyombo vya habari na hata mitandao ya kijamii nchini humo.
Waraka huo unaeleza masikito ya makatibu wakuu wastaafu wa chama Yusuph Makamba na Abdulrahman Kinana wakidai kuchafuliwa na kudhalilishwa na mtu anayejiita mwanaharakati na mtetezi wa serikali ya Rais John Magufuli.
Lakini siku chache baadae zikaanza kusambaa sauti zinazodaiwa ni mazungumzo kwa njia ya simu baina ya viongozi hao na wengine ikiwemo aliyekuwa Waziri wa Mazingira na Muungano January Makamba na Mbunge wa Mtama Nape Nnauye wakisikika kuzungumzia waraka huo na Rais Magufuli.
Siku ya Jumapili taarifa ya mabadiliko katika Baraza la mawaziri ilitolewa na Ikulu ya Tanzania huku January Makamba akifukuzwa kazi na nafasi yake kujazwa na George Simbachawene ambaye siku za nyuma alijiuzulu nafasi ya Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Hatua hiyo ikazua mjadala tena ikihusisha utenguzi wa Makamba na waraka wa makatibu wakuu wastaafu wa CCM na sauti za mazungumzo ya simu.
Siku ya Jumatatu Rais Magufuli amewaapisha Waziri Simbachewene na Naibu Waziri mpya wa Kilimo Hussein Bashe na katika hotuba yake fupi ambayo hata hivyo haiukuwa kama ilivyotarajaiwa na wengi kwamba angezumzia mjadala huo wa waraka, Magufuli amekosoa ucheleweshwaji wa katazo la mifuko ya plastiki wakati huo January Makamba akiwa Waziri.
Wachambuzi wa kisiasa wanasema kuwa ni hali ambayo imeteka hisia za wengi hasa kuhusu wasiwasi wa kuwepo kwa mpasuko ndani ya chama cha mapinduzi.
Baadhi ya wanachama wa CCM wamesikika kulaumu hatua ya viongozi hao wastaafu kuchapisha waraka huo ambao baadhi wanadai ni kama njama za kumhujumu Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM kuelekea uchaguzi Mkuu 2020.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC