Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 07:15

Wadau wahoji mswada wa mabadiliko ya sheria ya filamu Tanzania


Rais John Pombe Magufuli
Rais John Pombe Magufuli

Watengenezaji filamu na wanaharakati wa haki za kiraia Tanzania, wameulalamikia mswada unaopendekeza mabadiliko ya sheria zinazosimamia sekta ya filamu na michezo nchini humo.

Marekebisho ya mswada huo yanamtaka mtu yeyote au kampuni inayotengeneza filamu, kuwasilisha kanda zote zilizorekodiwa kwa bodi ya filamu kabla ya kufanya uhariri.

Mswada wa mabadiliko ya sheria namba 3 mwaka 2019 Tanzania kuhusu sekta ya filamu, unaotarajiwa kuasilishwa bungeni alhamisi hii kwa mjadala, unataka kampuni au mtu yoyote anayetengeneza filamu, matangazo ya biashara au Makala maalum, kwa kutumia picha za ndani ya Tanzania ni lazima aasilishe kanda zote zilizorekodiwa kwa bodi ya filamu kabla ya uhariri.

Wahusika wanahitajika kuambatanisha maelezo kuhusu sehemu zote walizorekodi kwenye video wakati wanapowasilisha video hizo kabla ya uhariri.

Wanahitajika pia kuasilisha nakala ya mwisho ya kazi yao ilimradi wametumia picha au video kuihusu Tanzania.

Wasanii, watengenezaji wa filamu na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kama vile Amnesty international, wanasema mswada huo una nia mbaya, lengo kubwa likiwa kukandamiza haki za kujieleza na kuchuja taarifa ambazo serikali inahisi zinachafua picha yake.

Daniel Nyalusi ni mtengenezaji filamu Tanzania. Amesema; “mtengenezaji filamu ni kama mwandishi wa habari. Mwandishi wa habari huandika habari za upekuzi, zinazohitaji usiri katika maandalizi yake. Kuna baadhi ya filamu tunazozitengeneza zinazohitaji usiri mkubwa katika maandalizi yake.

Ameongeza : "Unaweza ukatengeneza filamu inayoelezea jambo fulani katika jamii lakini kuna vitu Fulani kwanza unavificha. Ukisema maafisa wa serikali wakae chini waanze kutazama video zako kabla ya kuandaa, mfano rushwa, hawakuzuia kuandaa filamu yako”.

Mswada huo tayari umewasilishwa kwa kamati ya bunge ya katiba na sheria kwa hati ya dharura.

Watengenezaji wa filamu vile vile wanatakiwa kutoa hati miliki kwa serikali ya Tanzania, kutumia filamu zao kwa ajili ya utalii, na keuelezea raslimali zingine za Tanzania katika vyombo vya habari ikiwemo kimataifa bila malipo kwa mtengenezaji, ilimradi jina la washiriki kwenye filamu na wanaoandaa wanatajwa.

Wadau hao wa filamu wameutaja kama mswada potofu ambao waandalizi wake hawana ufahamu jinsi ya kazi ya filamu inavyotengenezwa, wakitaka mjadala kati yao na maafisa wa serikali kabla ya kupitishwa.

“nadhani kitu ambacho kinajaribu kulindwa na ambacho name naweza nikaunga mkono, ni utamaduni wetu kama watanzania. utamaduni wetu ni vigumu sana kutengeneza filamu za ushoga kwa mfano. Lakini kama sheria hii inalenga kuzuia ukweli kuzungumzwa, basi ni tatizo kubwa” ameongezea Nyalusi.

Atakayekiuka sheria, endapo itapitishwa, atatozwa faini ya aslimia 5 ya gharama yote aliyotumia kutengeneza filamu.

Sheria hii vile vile inawahusu watengenezaji wa filamu kutoka nchi zingine wanaotaka kufanya kazi yao nchini Tanzania.

Mswada unatarajiwa kuwasilishwa bungeni kwa mjadala, Alhamisi Juni 27 wiki hii.

Imetayarishwa na Mwendishi wetu Kennes Bwire, Washington DC

XS
SM
MD
LG