Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 15:38

Mwakyembe atoa sababu za kuanzishwa kanuni mpya Tanzania


Repoti ya 2018 ya Freedom House, inayoelezea hali ya Uhuru wa Habari Duniani.
Repoti ya 2018 ya Freedom House, inayoelezea hali ya Uhuru wa Habari Duniani.

WIZARA ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, imesema sababu zilizopelekea serikali kupitisha rasmi Kanuni za Maudhui mitandaoni, redioni na kwenye runinga ni kutokana na kuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili ya Kitanzania.

Serikali imesema kunaongezeko la maudhui hasi katika mitandao, redio na runinga. Pia vyombo vya habari vya magazeti navyo vikivunja sheria kwa kutozingatia weledi wa taaluma na kuchapisha habari zenye makosa ya kitaaluma.

Dkt Mwakyembe amesema hayo Ijumaa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya wizara hiyo kwa Mwaka 2018/19, kanuni hizo mpya zilizotungwa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta ya Mwaka 2010, zinazuia mitandao, runinga na redio kusambaza kauli chafu, matusi, picha za utupu na zenye maudhui yasiyofaa kwa watoto.

“Pia zinaingiza mitandao, redio na luninga kwenye mfumo rasmi wa kutambulika kisheria na kuwajibika kulipa. Zinamtaka kila mtumiaji mitandao awe na namba yake ya siri ili wajanja wasitumie kiurahisi chombo chake cha mawasiliano kutenda matendo hasi kinyume na sheria,” alisema Dkt Mwakyembe.

Kwa mujibu wa gazeti la Habari Leo waziri huyo alizifafanua kanuni hizo kuwa zinatambua Kiswahili na Kiingereza tu kuwa lugha rasmi zitakazotumika kwenye matangazo ya redio na runinga.

Alieleza kuwa kanuni hizo pia zinaweka muda maalumu kwa picha nyongevu za filamu au muziki wenye maneno yasiyo mazuri kwa watoto, zionyeshwe kwenye runinga katika muda maalumu.

“Tuliweka muda huo maalumu kuanzia saa nne usiku hadi saa 11:30 asubuhi, lakini wadau wamekuwa wakali, wanadai picha na nyimbo hizo zirushwe kuanzia saa 6:00 usiku wakati watoto wamelala na mwisho saa 11:00 asubuhi, kabla watoto hawajaamka,” alifafanua.

Alisema pamoja na kupitisha kanuni hizo ambazo tayari zimeanza kufanya kazi, pia wizara hiyo itaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kikabiliana na changamoto hiyo ya mmomonyoko wa maadili ya kitanzania. Alisema katika kufanikisha hilo, itaendelea kuhamasisha utengenezaji na uzalishaji wa maudhui ya ndani yanayozingatia maadili, mila na desturi za Mtanzania.

XS
SM
MD
LG