Uamuzi huo ulitangazwa na Spika wa bunge, Job Ndugai, katika hotuba yake ya kufunga kikao cha bajeti cha bunge la Tanzania.
Ndugai alisema kanuni za katiba ya nchi zinataka mbunge huyo anayewakilisha jimbo la Singida Mashariki kupitia Chadema avuliwe ubunge kwa kutotimiza masharti ya kuendeleza ushiriki wake katika shughuli za bunge.
Ndugai amesema mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi Tanzania ametumiwa taarifa rasmi kuelezea kuwa kuanzia hivi sasa Lissu amejiondoa ubunge na kiti chake cha ubunge kipo wazi. Hii ina maana Tume ya Uchaguzi, Tanzania, inaweza kuandaa uchaguzi mdogo kuziba nafasi hiyo.
Tundu Lissu ambaye alikuwa kiongozi wa upinzani bungeni kuanzia 2015 alikwenda nje ya nchi tangu aliposhambuliwa kwa bunduki nyumbani kwake mjini Dodoma Septemba 2017.
Mara baada ya kunusurika katika shambulizi hilo Lissu alisafirishwa hadi Nairobi, Kenya kwa matitabu ya dharura na baadaye nchini Ubelgiji ambako amekuwa akipata matibabu kwa miezi kadha sasa.
Mwanzoni mwa mwaka 2019 Tundu Lissu akiwa ameanza kupata nafuu kubwa alitembelea nchi kadha ikiwa ni pamoja na Uingereza, Marekani na kuilaumu serikali ya Tanzania kwa kushindwa kupata ufumbuzi kuhusu shambulizi dhidi yake.
Mwanasisasa huyo pia alitangaza mwezi uliopita kuwa anapanga kurejea nchini Tanzania Septemba mwaka huu, miaka miwili tangu kunusurika shambulizi la kutaka kumuua.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Washington, DC