“Kama isingekuwa Mnyezi Mungu maisha yangu yangeishia Dodoma siku ile niliposhambuliwa, lakini Mnyezi Mungu huyu wa uponyaji, Mnyezi Mungu alisema huyu hatakufa, naomba nimshukuru kwa hilo kwanza,” alisema mbunge huyo anayewakilisha jimbo la Singida mashariki nchini Tanzania ambaye amekuwa akipata matibabu katika hospitali moja ya Nairobi, Kenya.
Lissu ambaye pia ni Rais wa chama cha Wanasheria nchini Tanzania aliwashukuru madaktari, wauguzi, wafanyakazi wa kawaida na hospitali ya Nairobi, na hospitali ya mkoa wa Dodoma ambako alikimbizwa kwanza baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana.
Matamshi ya Lissu yalitangazwa kupitia mtandao wa chama chake cha siasa Chadema siku moja baada ya Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe kuelezea mjini Dar es salaam hali ya mwanasiasa huyo tangu afikishwe Nairobi kwa matibabu.
Lissu amewashukuru Watanzania kila walipo, akiongeza kuwa “… nao vilevile walipaza sauti makanisani, misikitini, kwenye mikutano yahadhara na kuniombea Mungu nipone.”
“Nafikiri sitakosea nikisema niko hai kwa sababu ya maombi ya mamilioni ya Watanzania,” alisisitiza.
Lissu amesema kuwa tangu kuwasili Kenya watu wengi sana wamekuja kumuona na kumpa pole hospitalini.