Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 23:07

Masha amuomba Magufuli kusaidia kupunguza hofu za Watanzania.


Lawrence Masha
Lawrence Masha

Aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya ndani Tanzania, Lawrence Masha ameshangazwa na msimamo wa serikali kukataa msaada wa uchunguzi kutoka nje kufuatia watu kadhaa kupigwa risasi, miili ya maiti kuokotwa katika fukwe ya bahari na wengine kupotea.

"Nilishangaa kuona Waziri wa Mambo ya ndani, (Mwiguilu Nchemba) akikataa msaada wa uchunguzi kutoka nje ya nchi. Nikajua hawana nia njema. Sio jambo geni mbona viongozi wetu wamefanya training nje ya nchi?

Masha, ambaye ni mwanasheria alikuwa akizungumza Ijumaa mbele ya waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika leo makao makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kinondoni, Dar es Salaam.

“Utaratibu wa Serikali ya Tanzania kuruhusu wachunguzi wa taasisi za nje za kiuchunguzi si mgeni; na wala kuwapa nafasi wachunguzi wa mataifa ya nje kwenye matukio yanayotokea sasa, si fedheha kwa serikali na nchi,” amesema Masha ambaye pia ni wakili wa Mahakama Kuu, na kiongozi mwandamizi wa Chadema.

“Marekani imeendelea lakini huchukua wachunguzi wa nje muda mwingine, mfano Uingereza na sehemu nyingine, sio kwamba wao hawawezi kazi,” amesema Masha.

Tukio la kwanza ni kuuliwa kwa risasi kwa Padre Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Zanzibar, la Februari 17, 2013, ambalo lilichunguzwa na wapelelezi wa Shirika la Upelelezi la Marekani – Federal Bureau of Investigation (FBI).

Tukio jingine lilichunguzwa na wapelelezi wa nje ya Tanzania, ni la mapema Agosti 2013 la kumwagiwa tindikali vijana wawili wa kujitolea wa Uingereza waliokuwa wakifanya kazi ya ualimu visiwani Zanzibar.

Katie Gee, mwenye umri wa miaka 22, na Kirstie Trup 18, walikuwa wakifundisha watoto yatima mjini Zanzibar, walipokutwa na kadhia hiyo walipowasili tu hotelini kwa ajili ya chakula cha usiku.

Makachero wa Scotland Yard, kikosi mashuhuri kwa uchunguzi wa matukio ya jinai cha Uingereza, waliingia nchini kwa siri na kuchunguza tukio hilo.

Masha amesema uchunguzi wa vyombo vya nje utaipa heshima Tanzania kuwa imejenga imani kwa umma na jumuiya ya kimataifa kwamba haina cha kuficha katika matukio hayo ya uhalifu.

Kumekuwa na hisia tofauti kufuatia matukio ya uhalifu ambayo mpaka sasa wananchi wanadadisi hatua ambazo jeshi la polisi imeweza kuzichukua kukomesha vitendo hivyo.

Masha amemuomba rais awaagize makamanda wake watafute msaada, kwani leo hii watanzania wanaishi kwa hofu.

"Sisi watanzania maswala ya kiitikadi hajawahi kutusumbua wala udini. lakini sasa hivi watu wanayo hofu, " amesema Masha.

Ameongeza kuwa ni majuzi tu mzungu aliyekuwa anasaidia nchi kupunguza uwindaji wa Tembo, alipigwa risasi akauawa.

"Watu wanaogopa kutoka nje, watu wanaogopa kutembea usiku sasa hivi watu wanaogopa hata kuongea," amesema.

Amemtaka Rais Magufuli awaombe makamanda wake wapokee msaada wa uchunguzi kwani siyo fedheha.

Pia amewataka wananchi waendelee kumuombea Mbunge wa Singida Tundu Lissu ambaye bado yuko Kenya kwa matibabu baada ya watu wasiojulikana kumpiga risasi alipowasili nyumbani kwake Dodoma Tanzania ambako alikuwa akihudhuria kikao cha Bunge.

XS
SM
MD
LG