Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 27, 2024 Local time: 06:08

Tanzania : Mawakili wa Eric Kabendera wahoji tuhuma mpya za uhujumu uchumi dhidi yake


Eric Kabendera akiwa mahakamani Jumatatu Agosti 5, 2019.
Eric Kabendera akiwa mahakamani Jumatatu Agosti 5, 2019.

Mwandishi wa habari nchini Tanzania Erick Kabendera Jumatatu, amepandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka mapya ya uhujumu uchumi baada ya kuzuiliwa na polisi kwa zaidi ya siku saba.

Mashtaka mapya yanamtuhumu kwa kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu uchumi nchini na kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya Sh. milioni mia moja za Kitanzania.

Kosa jingine ni la utakatishaji fedha zenye thamani ya zaidi ya Sh. millioni mia moja na sabini.

Muungano wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) wameeleza kuwa hapo awali alikamatwa na kuhojiwa kwa uchochezi na uchapishaji wa habari za uongo. Lakini Jumatatu madai yaliyotolewa mahakamani dhidi yake ni mapya kabisa na yamezua maswali mengi juu ya hayo. Moja ni kwa nini alikuwa hajahojiwa juu ya tuhuma hizo dhidi yake zilizoletwa leo.

Mtandao huo umeripoti pia kuwa Kabendera anadaiwa kuyafanya makosa hayo kati ya Januari 2015, na Julai mwaka 2019 jijini Dar es Salaam, kwa kushirikiana na watu ambao hawakuwepo mahakamani.

Kwa mujibu wa wakili wake makosa yote hayo hayana dhamana. Mtuhumiwa hakutakiwa kujibu lolote mahakamani kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo. Mawakili wake wameondoa ombi la dhamana kutokana na mashtaka hayo mapya.

Kabendera anayeandikia magazeti ndani na nje ya Tanzania, alikamatwa Jumatatu, Julai 29, wiki iliyopita na watu waliojitambulisha kuwa ni maofisa wa polisi. Katika mkutano na vyombo vya habari, kamanda wa polisi kanda maalum ya mji wa Dar, Lazaro Mambossasa, amesema kuwa mshukiwa huyo alikaidi agizo la polisi la kufika mbele yao kwa ajili ya mahojiano.

Akizungumza na wanadishi wa habari punde baada ya Kabendera kusomewa mashtaka, wakili wake Jebra Kambole amesema: “Wakati Erick anakamatwa siku ya kwanza aliambiwa kosa lake ni la uhamiaji, akapelekwa kwenye mamlaka za uhamiaji, akahojiwa, pasipoti yake ikachukuliwa.

Uhamiaji wakamkabidhi kwa jeshi la polisi makao makuu (central) ya Jeshi la Polisi wakamhoji kwa makosa ya uchochezi. Kuanzia hapo hajawahi kuhojiwa kwa makosa mengine zaidi ya hayo.”

“Tunachofanya sasa, ni kuangalia upelelezi unafanyika kwa wakati,” ameeleza wakili huyo. Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa Agosti 19 mwaka huu.

”Mwandishi huyu aliitwa, hakutekwa lakini kwa ujeuri alikaidi wito huo… Kimsingi pengine iwapo angewasili angehojiwa na kuachiliwa,” alisema Mambossasa

XS
SM
MD
LG