Tanzania na Uganda wasaini mkataba wa ujenzi wa bomba la mafuta

Rais Yoweri Museveni wa Uganda akilakiwa na mwenyeji wake Rais John Magufuli wa Tanzania mara baada ya kuwasili Chato, Geita. Picha kwa Hisani ya Global Publishers TV Tanzania.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Jumapili Septemba 13, 2020 amewasili uwanja wa ndege wa Chato mkoa wa Geita na kupokelewa na mwenyeji wake, Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli ili kushuhudia utiaji saini mkataba wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta.

Sherehe za utiaji saini zimefanyika katika uwanja wa idege wa Chato huku kukiwa na tahadhari zote za kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19).

Viongozi hao wawili wamekubaliana asilimia 60 ya faida ya itakayopatikana katika mafuta hayo itakwenda kwa Tanzania huku asilimia 40 ikienda kwa Uganda.

Bomba hilo la mafuta linatarajiwa kujengwa kutoka mji wa Hoima, Uganda hadi eneo la chongoleani mjini Tanga Tanzania.

Mkataba umetiwa saini na mawaziri wa nishati kutoka mataifa hayo mawili na kushuhudiwa na marais John Magufuli wa Tanzania na Museveni wa Uganda mjini Chato.

Rais Museveni alisema kitu muhimu ni kuanza kwa mradi huo aliosema ulicheleweshwa kutokana na mlipuko wa COVID-19.

Museveni ameeleza uwekezaji wa bomba hilo la mafuta utagharimu dola bilioni 4 za Marekani.

Naye rais Magufuli amesema mradi huo utaimarisha uchumi wa nchi hizo na eneo lote la Afrika Mashariki na Kati.