Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 15:03

Mwanadiplomasia Membe aingia upinzani kupambana na Magufuli


Bernard Membe
Bernard Membe

Mpaka mwezi Julai mwaka 2020 Bernard Kamillius Membe alikuwa mwanachama wa miaka mingi katika chama tawala cha Tanzania, CCM, na mwanasiasa aliyewahi kushika wadhifa wa juu na muhimu katika serikali za chama hicho.

Chini ya serikali ya CCM Membe alishika nyadhifa mbali kama mwanadiplomasia, waziri mdogo hadi nafasi adhimu ya waziri wa mambo ya nje Tanzania kwa miaka 14 katika utawala wa Rais wa zamani Jakaya Mrisho Kikwete.

Hata hivyo kufuatia kashfa ya udukuzi wa mawasiliano ya simu mwaka 2019 ambapo Membe na wanasiasa wengine walidukuliwa wakimsema Rais John Magufuli alijikuta taratibu akitengwa ndani ya chama hicho.

Tija yake katika chama ilibadilika zaidi pale Kamati Kuu ya CCM iliposimamisha uanachama wake Februari 2020 kwa kukiuka maadili ya uongozi. Membe alikanusha madai dhidi yake akisema kuwa kosa lake ilikuwa kuonyesha nia ya kutaka kupambana na Rais Magufuli katika kuwania ugombea urais kupitia CCM katika uchaguzi wa 2020. Mwezi Julai Membe alirudisha rasmi kadi ya CCM na siku chache baadaye akajiunga na chama cha upinzani cha ATC Wazalendo.

TUMEya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imemteua Bernard Membe kuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia ACT-Wazalendo na mgombea mwenza, Profesa Omar Fakih Hamad, kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28, 2020. Membe ni mgombea wa tisa kuteuliwa.
TUMEya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imemteua Bernard Membe kuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia ACT-Wazalendo na mgombea mwenza, Profesa Omar Fakih Hamad, kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28, 2020. Membe ni mgombea wa tisa kuteuliwa.

Wakati wote wa utawala wa Rais Magufuli baada ya uchaguzi wa 2015 Membe alisemekana kuwa mpinzani wa chini chini wa rais huyo mpya ndani ya chama cha CCM. Haikuwa ajabu kwa wachumbuzi wa siasa kwamba hatimaye Membe aliondoka CCM na kuhamia chama cha upinzani.

Mara baada ya kujiunga na ACT Membe, mwenye umri wa miaka 66, aliteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera ya chama kama mgombea urais dhidi ya Rais Magufuli ambaye anawamia awamu ya pili ya utawala.

Bernard Kamillius Membe, alizaliwa mwaka 1953 katika mkoa wa Lindi, kusini mwa Tanzania. Baada ya elimu ya msingi na sekondari Membe alijiunga na chuo kikuu cha Dar es salaam ambako alipata shahada ya sayansi ya siasa na baadaye akaenda chuo kikuu cha John Hopkins mjini Washington, D.C Marekani ambako alisomea uhusiano wa kimataifa. Mwaka 1992 serikali ya Tanzania ilimpeleka Membe katika ubalozi wa Tanzania mjini Ottawa, Canada, kama mshauri wa balozi.

Mwaka 2000 alianza kujitoa katika utumishi wa serikali na kuingia katika siasa kwa kuchaguliwa kama mbunge wa jimbo la Mtama, mkoani Lindi. Wananchi wa jimbo hilo walimchagua awamu mbili nyingine kuwa mbunge wao mwaka 2005 na 2010.

Alishika wadhifa wa kwanza kama naibu wa waziri wa mambo ya nje katika serikali ya rais Jakaya Kikwete mwaka 2005 na baadaye kama naibu waziri wa madini na nishati mwaka 2006. Mwaka 2007 Bernard Membe aliingia katika wadhifa wa juu na wa kuonekana zaidi duniani alipoteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje kufuatia uteuzi wa aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wakati huo Asha Rose-Migiro kama katibu mkuu msaidizi katika Umoja wa Mataifa mjini New York.

Membe alikuwa mmoja wa wana CCM kadha waliowania urais kupitia chama hicho mwaka 2015 na alikuwa miongoni mwa wanasiasa walioonekana kuwa na nafasi nzuri. Baadhi ya wachambuzi walisema wakati huo kwamba Membe alikuwa chaguo la rais aliyekuwa anaondoka madarakani Jakaya Kikwete.

Hatimaye, CCM ilimteua John Pombe Magufuli kuwa mgombea wa CCM na akashinda uchaguzi mkuu Oktoba 2015. Tangu wakati huo, vyanzo vya habari na wachambuzi, wanasema uhusiano wa Rais Magufuli na Bernard Membe uliharibika.

Kama mgombea urais kupitia ACT Wazalendo Bernard Membe amejikuta katika kundi la wagombea wengine 15 wa urais. Hata hivyo, yeye na mgombea mwingine wa chama cha Chadema, Tundu Lissu, wanaonekana kuwa na angalau nafasi ya kupambana na Rais Magufuli.

Membe ameonyesha nia ya kutumia uzoefu wake kama mwanadiplomasia wa ngazi za juu Tanzania kuonyesha tofauti yake na Rais Magufuli ambaye katika miaka yake mitano madarakani hajaonyesha juhudi kubwa kuendeleza uhusiano wa kimataifa.

Bernard Membe
Bernard Membe

Membe anapeperusha sera za ACT Wazalendo kwa kauli mbiu, Kazi na Bata, ikiwa na maana kuwaletea wananchi wa Tanzania taifa linalothamini kazi lakini na maisha bora pia.

Ilani ya ACT-Wazalendo inasisitiza pia elimu ya juu kwa wote, bima ya afya kwa wote, maji safi na salama kwa kila mtanzania na kilimo cha kimapinduzi.

XS
SM
MD
LG