Ukali wake katika utendaji kazi ulimfanya akapewa jina la ‘Bulldozer’ lakini pia ameonyesha sura ya kuwa mtetezi wa wanyonge kutokana na sera za kupigania haki ya taifa la Tanzania kusimamia rasilimali zake ili zifaidishe wananchi.
Anaingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi akiwa na mlolongo wa kile ambacho chama chake cha CCM ba wanaomwunga mkono wanasema ni mafanikio makubwa katika awamu yake ya kwanza ya uongozi wake.
Lakini mafanikio yake pia yanatumiwa na wapinzani kama silaha dhidi yake katika uchaguzi huu. Wapinzani wake wakuu Tundu Lissu wa Chadema na Bernard Membe wa ACT Wazalendo wanamkosoa vikali kwa kufanya miradi ya kitaifa kama miundo mbinu kwa maamuzi yake mwenyewe bila kupitisha miradi hiyo katika bunge la taifa.
Magufuli ambaye ataingia umri wa miaka 61 siku moja baada ya uchaguzi, alizaliwa Chato, magharibi ya Tanzania mwaka 1959. Baada ya masomo ya shule ya msingi na sekondari alihitimu shahdada ya kwanza toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alirejea tena chuoni hapo kama mwalimu na hatimaye, kuendelea na masomo yake hadi shahada ya uvamivu au PhD.
Alianza siasa mwaka 1995 kwa kuchaguliwa kama mbunge katika chama cha CCM, na tangu wakati huo Magufuli amekua katika baraza la mawaziri la serikali za Tanzania kuanzia utawala wa marehemu rais Benjamin Mkapa hadi Jakaya Kikwete.
Mwaka 2015 aliibuka kutoka chini katika kundi kubwa la wanasiasa waliowania ugombea wa chama cha CCM na hatimaye kushinda uchaguzi wa mwaka huo dhidi ya mgombea wa muungano wa upinzani uliojulikana kama UKAWA Waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa .
Magufuli kwa wengi anaelezewa kuwa ni mchapa kazi na mkali na mwenye kuweza kuchukua hatua wakati wowote na tangu aingie madarakani amechukua hatua kama vile kuwafukuza kazi watumishi wa umma wakati wowote aliohisi hawatimizi wajibu wao, akiwa na msemo wa ‘kutumbua majipu’ na ‘hapa kazi tu’.
“Nachukia wezi, kwa kweli watakoma. Mwizi anatoka Ulaya au anatoka West, East, South mwizi ni mwizi tu, lazima waule wa chuya, kwa hiyo tutaendelea kubana mianya yote”alisema rais Magufuli.
Magufuli pia anajulikana kwa kupambana na ufisadi akitaja kwamba yuko tayari hata kwenda kinyume na chama chake na bila kujali wenye majina na uwezo kuondolewa au kushitakiwa wanapogundulika wamehusika na vitendo hivyo.Alitangaza pia vita na madawa ya kulevya nchini humo.
Moja ya maswala anayosifiwa Magufuli ni jinsi alivyopigania haki ya uchimbaji madini na makampuni ya nje ya Acacia na kampuni mama Barrick hadi pande hizo mbili zikakubaliana Oktoba 2019 kulipa dola milioni 300 na kuipatia serikali ya Tanzania asilimia 16 katika kampuni yao iliyopewa jina la Twiga.
Katika kile kilichoonekana na makundi ya haki za binadamu kama serikali ya Magufuli kuzuia uhuru wa habari utawala huo umefungia magazeti kadha. Amnesty International inasema magazeti ya lugha ya Kiswahili Raia Mwema, Mawio na Mwanahalisi yote yalifungiwa kwa muda baada ya kuchapisha nakala tofauti za kumkosoa rais.
Wakati wa janga la Corona Magufuli aliongoza nchi yake katika mwelekeo tofauti na nchi nyingine huku akisema mwezi Mei 2020 kuwa Corona imekwisha nchini humo kwa sababu ya maombi, na kuondoa masharti mengi ya kujikinga na virusi hivyo ingawa tahadhari zinaendelea kuchukuliwa.
Tanzania haijatoa taarifa yoyote juu ya kesi za virusi vya corona tangu Aprili 29, 2020. Katika hesabu ya mwisho, kulikuwa na kesi 509 zilizoripotiwa na vifo 21 nchini humo, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).
Rais Magufuli atakuwa anaongoza chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu akiwa na makamu wake Samia Suluhu na akiendelea na nia ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda huku akijivunia nchi hiyo kuingia uchumi wa kati mwaka huu kwa mujibu wa benki ya Dunia.