Chama cha NCCR Mageuzi kimefanya mkutano wake mkuu maalum Ijumaa, kwa ajili ya kumchagua mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar.
Vyama vinne ikiwemo CCM wagombea wake wameshachukua fomu katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC na kuacha uwanja kwa vyama vingine ambavyo vinaendelea kujipanga.
NCCR Mageuzi ambacho katika miaka ya hivi karibuni kiliwakaribisha wabunge watatu waliokuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinaendelea na mkutano wake na kinatarajiwa kupitisha jina moja miongoni mwa wagombea watatu waliojitokeza kuwania nafasi hiyo, inaripoti Mtandao wa Habari wa Global Publishers TV Tanzania.
Mkuu wa idara ya mawasiliano na uenezi kwa umma wa chama hicho, Edward Simbeye, amesema mkutano huo pia utapitisha jina la mgombea wa kiti cha urais Zanzibar ambapo ni mwanachama mmoja tu aliyejitokeza kwenye nafasi hiyo.
Suala la maridhiano na ushirikiano kuelekea kwenye uchaguzi huu miongoni mwa vyama vya upinzani limeendelea kujitokeza pia katika mkutano huu. Wimbo huu wa ushirikiano ambao bado haijajulikana namna utakavyopatiwa ufumbuzi, imekuwa mada inayotajwa mara zote tangu kuanza kwa mchakato huu wa uchaguzi.
Huku hayo yakiarifiwa, naibu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye tayari ameteuliwa na chama chake kuwa mgombea wa urais katika uchaguzi ujao, ameitwa katika mahakama ya Kisutu anakokabiliwa na kesi za uchochezi.
Mahakama hiyo imemwamuru kufika mahakamani hapo Agosti 31 akiwa na wadhamini wake ili kujua hatma ya kesi yake. Hatua hiyo inatokea baada ya wadhamini hao kushindwa kutokea mahakamani hapo kwa muda mrefu, wakati Lissu akiwa ughaibuni kwa matibabu.
Wakati huo huo, Chama cha ACT Wazalendo kitawatambulisha wagombea wa urais wa pande zote mbili kwa wanachama wake wa Zanzibar siku ya Jumapili.