Rais John Pombe Magufuli anawania awamu ya pili ya uongozi akiwakilisha chama tawala cha CCM wakati Zanzibar itapata rais mpya baada ya Rais Ali Mohammed Sheni kumaliza awamu mbili katika uongozi.
Rais Magufuli anakabiliwa na ushindani kutoka kwa wagombea 15 wa upinzani lakini miezi miwili kabla uchaguzi washindani wanaojitokeza kuwa wakubwa kwa Rais Magufuli huenda wakawa Tundu Lissu wa chama cha Chadema na Bernard Membe ambaye anawakilisha chama cha ACT Wazalendo. Membe alikuwa waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Tanzania wakati wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete alifukuzwa kutoka chama tawala cha CCM na kujiunga na ACT mwezi Julai.
Katika visiwa vya Zanzibar chama tawala cha CCM kinawakilishwa na Hussein Mwinyi aliyekuwa waziri wa ulinzi katika serikali ya awamu ya kwanza ya Rais Magufuli, atapambana na Maalim Seif Shariff Hamad wa ACT Wazalendo ambaye anawania urais kwa mara ya sita sasa.
Mamia ya wagombea wakiwakilisha vyama mbali mbali watakuwa wanawania nafasi katika bunge la Jamhuri lenye jumla ya wajumbe 392, lakini viti vinavyogombaniwa katika uchaguzi huu ni 264, viti vilivyobaki ni vya kuteuliwa. Baraza la wawakilishi la Zanzibar lina viti 88, na 50 kati ya hivyo vinagombaniwa katika uchaguzi huu.
Mamia ya wagombea watakuwa wanawania nafasi za udiwani katika halmashauri na miji mbali mbali nchini humo. Kulingana na Tume ya Uchaguzi kuna nafasi za madiwani 5350 katika nchi nzima.
Tume ya Uchaguzi inasema jumla ya watanzania millioni 29 wamejiandikisha kupiga kura nchini humo mwaka huu idadi ambayo huenda ikawa ni kubwa kuliko yote kuwahi kujiandikisha kupiga kura katika historia ya Tanzania.
Uchaguzi mkuu Tanzania hufanyika kila miaka 5. Mshindi anatakiwa kupata wingi tu wa kura kuliko mgombea anayemfuatia. Mgombea urais anatakiwa kikatiba kuwa mzaliwa wa Tanzania mwenye umri usiopungua miaka 40.