Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 06:21

Tume ya uchaguzi yatupilia mbali pingamizi la Lissu


Mgombea urais kupitia chama cha CHADEMA Tundu Lissu akizungumza baada ya kuteuliwa kuwa mgombea katika mkutano mkuu wa chama hicho Dar es Salaam, Tanzania, Aug. 4, 2020.
Mgombea urais kupitia chama cha CHADEMA Tundu Lissu akizungumza baada ya kuteuliwa kuwa mgombea katika mkutano mkuu wa chama hicho Dar es Salaam, Tanzania, Aug. 4, 2020.

Tume ya taifa ya uchaguzi ya Tanzania (NEC) imetupilia mbali pingamizi la mgombea wa chama cha upinzani cha CHADEMA Tundu Lissu aliyowasilisha dhidi ya mgombea wa chama tawala cha CCM Rais John Magufuli na mgombea wa urais kupitia chama cha CUF Profesa Ibrahim Lipumba.

“Tume imejiridhisha baada ya kupitia sababu za pingamizi zote mbili pamoja na utetezi uliotolewa imejiridhisha kuwa Dr John Pombe Joseph Magufuli mgombea wa CCM amerejesha fomu zake ambazo zimeambatanishwa na picha kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo ya tume ya taifa ya uchaguzi. Hivyo tume ya taifa ya uchaguzi imejiridhisha kwamba pingamizi hizo hazina msingi wa kisheria na imezitupilia mbali.” Ilieleza sehemu ya taarifa ya tume hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wake Dr.Wilson Mahera.

Tundu Lissu aliwawekea pingamizi wagombea Rais Magufuli na Profesa Lipumba, akidai wagombea hao wamekiuka sheria za uchaguzi katika kifungu namba 38(4)b cha sheria ya uchaguzi.

Lissu aliandika pia katika ukurasa wake wa Twitter kwamba hakujawa na pingamizi ya aina yeyote ile iliyowekwa dhidi yake.

Hayo yanajiri wakati baadhi ya wagombea wa upinzani katika ngazi za ubunge na udiwani wakilalamikia vitendo mbali mbali dhidi yao wasiweze kuidhinishwa kama wagombea, ikiwa ni pamoja na fomu zao kubadilishwa na wakurugenzi wanaopokea fomu hizo na hata kupokonywa fomu za uchaguzi na watu wasiojulikana wakati wakielekea kwenye ofisi ya tume ya uchaguzi.

Viongozi wa vyama hivyo wasema wagombea wao wengi wamelazimika kukata rufaa kwa tume ya uchaguzi katika mazingira magumu.

Viongozi wa upinzani wametoa wito wa utendaji haki kwa wagombea wote huku mkurugenzi wa Tume akionya vyombo vya habari vinavyotangaza kwamba kuna waliopita bila kupingwa wakati tume hiyo haijatoa taarifa yeyote juu ya zoezi hilo.

Tume ya Uchaguzi haijatoa tamko lolote kuhusu malalamiko ya upinzani kwamba wagombea wao wanaenguliwa kutoka katika ushindani kwa sababu zisizo za msingi.

XS
SM
MD
LG