Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 19:17

Wapinzani Tanzania walalamika kuenguliwa kwa mamia ya wagombea wao


Benson Kigaila
Benson Kigaila

Vyama kadha vya upinzani nchini Tanzania vimelalamika kwamba mamia ya wagombea wao wameenguliwa katika mchakato wa kuidhinisha ushiriki wao katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28. 

Vyama hivyo vimetoa wito kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushughulikia malalamiko yao ambayo yamewasilishwa rasmi baada ya maafisa katika ngazi za chini kuondoa wagombea wengi wa ubunge na udiwani kutoka vyama vya upinzani kuliko ilivyo kwa wagombea wa chama tawala cha CCM.

Naibu Katibu Mkuu wa chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA nchini humo, Benson Kigaila, amesema hadi kufikia Alhamisi wagombea wao katika nafasi za ubunge katika majimbo 57 na wagombea udiwani 642 wameenguliwa katika mazingira tata.

Kigaila alieleza kisa cha mgombea mmoja aliyeomba fomu ya kukata rufaa na badala yake Mkurugenzi akaondoka na kufunga ofisi huku mgombea akilazimika kusubiri ofisini kutwa nzima bila mkurugenzi kurejea ofisini hapo.

Malalamiko ya aina hiyo yamejirudia katika majimbo mbali mbali ya uchaguzi nchini humo kwa wagombea kutoka vyama vya upinzani.

Kigaila amesema kuwa wamekwishatoa taarifa kwa Tume ya taifa ya Uchaguzi na kutaka uchunguzi ufanywe ili wagombea wao warejeshwe katika ugombea.

Ibrahim Lipumba kiongozi wa chama cha CUF
Ibrahim Lipumba kiongozi wa chama cha CUF

Nacho chama cha wananchi CUF kupitia kwa Mwenyekiti wake Profesa Ibrahim Lipumba wao kinasema kimepokea taarifa za wagombea wao kuwekewa pingamizi na baadhi ya maeneo wagombea wao kuporwa fomu za ugombea na watu wasiojulikana.

“kuna watu wamewekewa pingamizi kuna kwingine watu wamevamiwa wamenyang’anywa fomu,” alisema Professa Lipumba.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera Charles, aliithibitishia VOA kwamba wamepokea malalamiko na mapingamizi na kwamba bado wanayafanyia kazi na kusema kuwa katika kipindi cha siku nanewatatoa maamuzi.

“Hatujasema ni hujuma mpaka itakapothibitishwa ni hujuma, lakini kuna changamoto. Utakuta wengine ni kweli, wengine utakuta hawajatekeleza vizuri masharti ya uteuzi,” alisema Dr. Mahera.

Katika hatua nyingine NEC imetupilia mbali pingamizi dhidi ya mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi Rais John Magufuli na mgombea urais wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba lililowekwa na mgombea urais wa CHADEMA Tundu Lissu kuwa fomu zao zilijazwa kimakosa na hawakurudisha fomu hizo kwa kufuata masharti. Taarifa hiyo imeeleza kuwa wagombea hao walikidhi matakwa ya kisheria katika fomu zao na kwamba wanaendelea kuwa wagombea

XS
SM
MD
LG