Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 19:45

Tanzania yafafanua kanuni ya ushirikiano na vyombo vya nje


Msemaji wa TCRA Tanzania akiongea na vyombo vya habari.
Msemaji wa TCRA Tanzania akiongea na vyombo vya habari.

TCRA yasema haijakataza matangazo kuendelea ila vyombo vya ndani vipate vibali ndani ya muda wa siku saba kuendelea kurusha matangazo ya vyombo vya kimataifa

Katika ufafanuzi iliotoa Jumatano kuhusu sheria yake ya ushirikiano wa vyombo vya habari vya ndani ya Tanzania na vile vya nje Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema vyombo vya Tanzania vinaweza kuendelea kurusha matangazo ya nje wakati vinatafuta vibali katika muda wa siku saba.

Akizungumza na vyombo va habari mjini Dar es Salaam, msemaji wa TRCA alisema "...Sisi hatujakataza mikataba iliyokuwa inaendelea kutumika isitumike. Tunaomba vyombo vyote, kuwapa taarifa kwamba muwasilishe maombi yenu na mikataba hiyo inayoendelea kwa (TCRA) katika kipindi cha siku saba, lakini endeleeni kutangaza ili kuhakikisha kwamba ile mikataba yenu iliyokuwepo inaendelea kutekelezeka. Lakini ndani ya hizo siku saba muwe mmeleta hiyo mikataba (TCRA) ili kupata vibali kwa ajili ya kuendelea na kazi hizo."

Ufafanuzi huo umekuja baada ya taharuki iliyotokea kuanzia mwanzoni mwa wiki, TCRA ilipotangaza ongezeko la kipengele katika sheria ya mwaka 2018 iliyofanyiwa marekebisho 2020 kutaka vyombo vya ndani vipate vibali ili kurusha matangazo ya vyombo vya kimataifa.

Sheria hiyo ilikosolewa ndani na nje ya Tanzania kwamba ina lengo la kuzuia upatikanaji wa matangazo ya vyombo vya nje kama vile VOA, BBC na DW hasa wakati huu ambapo Tanzania inaelekea katika uchaguzi mkuu mwezi Oktoba.

Baadhi ya televisheni na radio zilisimamisha mara moja urushaji wa matangazo ya vyombo vya nje na badala yake kuanza mara moja utaratibu wa kupata kibali kutoka TCRA. Lakini ripoti kutoka ndani ya Tanzania zinasema baadhi ya stesheni zinaendelea kurusha matangazo hayo.

Ufafanuzi wa TRCA Jumatano hata hivyo haujaweka bayana siku hizo saba zinaisha lini, na endapo stesheni imeshindwa kupata kibali inaweza kuomba kuongezewa muda au italazimika kusimamisha matangazo ya vyombo vya nje.

Mamlaka hiyo imesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kusimamia maudhui ya nje yanayorushwa mbashara nchini Tanzania na kwamba huo ni utaratibu wenye lengo la kuleta ufanisi katika usimamizi wa matangazo.

Hata hivyo wakosoaji wanasema hatua hiyo inaonekana kuwa nyingine katika mlolongo wa sheria tangu mwaka 2018 zinazolenga kudhibiti upatikanaji wa habari nchini Tanzania.

Hivi karibuni Radio Free Africa yenye makao yake makuu Mwanza ilitakiwa kufika mbele ya TCRA kujieleza kwanini isichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka kanuni za utangazaji kufuatia mahojiano iliyorusha wakati wa kipindi cha BBC Swahili baina ya BBC na kiongozi wa upinzani Tundu Lissu wa chama cha CHADEMA.

XS
SM
MD
LG