Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 16:48

Russia yafanya mashambulizi zaidi katika miundombinu, na makazi ya watu Ukraine


FILE - Picha ya satellite iliyosambazwa na Maxar Technologies inaonyesha kituo cha umeme kimeharibiwa Kyiv, Ukraine, Oct. 12, 2022, kufuatia shambulizi la Russia.
FILE - Picha ya satellite iliyosambazwa na Maxar Technologies inaonyesha kituo cha umeme kimeharibiwa Kyiv, Ukraine, Oct. 12, 2022, kufuatia shambulizi la Russia.

Majeshi ya Russia Jumamosi  yamefanya mashambulizi zaidi ya hapa na pale  nchini Ukraine, yakilenga miundombinu ambayo inasambaza umeme nchini na katika makazi ya watu.

Gavana wa Kyiv Oleksiy Kuleba alisema shambulizi hilo limeharibu kituo kikuu cha umeme katika mji mkuu wa Ukraine, lakini hakuna taarifa za mtu yeyote kuuwawa, na eneo lililoshambuliwa halikutajwa.

Russia yafanya shambulizi la angani huko Bila Tserkva, kusini magharibi ya Kyiv Octoba 5, 2022. Ndege isiyokuwa na rubani iliyotengenezwa Iran inadaiwa kufanya shambulizi hilo.
Russia yafanya shambulizi la angani huko Bila Tserkva, kusini magharibi ya Kyiv Octoba 5, 2022. Ndege isiyokuwa na rubani iliyotengenezwa Iran inadaiwa kufanya shambulizi hilo.

Kyrylo Tymoshenko, naibu mkuu wa ofisi ya rais wa Ukraine, aliwasihi wakaazi wa eneo la Kyiv na watu katika miji mitatu jirani kupunguza matumizi ya umeme wakati wa saa za jioni ambapo mahitaji yako juu.

Shambulizi hilo katika kituo cha kusambaza umeme limetokea saa kadhaa baada ya maafisa wa Ukraine kusema Russia ilifyatua makombora katika makazi ya watu huko Nikopol, kusini mashariki mwa Zaporizhzhia.

Yevhen Yevtushenko, mkuu wa utawala wa kijeshi wa wilaya ya Nikopol, alisema watu watano walijeruhiwa katika shambulizi la Jumamosi asubuhi katika mji huo. Alisema mashambulizi hayo yalilenga kuleta “uharibifu mkubwa kwa raia.”

Warusi wauawa katika uwanja wa mafunzo

Wakati huo huo takriban wanajeshi 11 wa Russia waliuawa na wengine zaidi ya 15 kujeruhiwa Jumamosi wakati wanajeshi wawili wa kujitolea wa Russia walipofyatua risasi katika uwanja wa mafunzo ya kulenga shabaha huko kusini magharibi katika mkoa wa Belgorod karibu na Ukraine, kulingana na wizara ya ulinzi ya Russia.

Russia ikifanya mazoezi ya shabaha kwa vikosi vyake katika mikoa yake mitatu Rostov, Belgorod na Kursk inayopakana na Ukraine.
Russia ikifanya mazoezi ya shabaha kwa vikosi vyake katika mikoa yake mitatu Rostov, Belgorod na Kursk inayopakana na Ukraine.

Wizara ya Ulinzi Russia ilisema askari hao wawili wakujitolea walikuwa wanatokea taifa la zamani la Soviet na waliuawa baada ya kujibiwa shambulizi lao, ikieleza tukio hilo kuwa ni shambulizi la kigaidi.

“Wakati wa mafunzo ya namna ya kutumia silaha yakitolewa kwa watu waliojitolea wakiwa na utashi wa kushiriki katika operesheni maalum ya kijeshi (dhidi ya Ukraine), magaidi hao walifyatua risasi wakitumia silaha ndogo kwa wafanyakazi wa kikundi hicho,” RIA ilieleza taarifa ya jeshi la ulinzi ilisema hayo.

Baadhi ya vyombo vya habari huru vya Russia vimerepoti idadi kubwa ya waliouwawa katika tukio hilo.

Oleksiy Arestovych, mshauri wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, alisema katika mahojiano kuwa washambuliaji hao katika tukio hilo la kigaidi walikuwa wametokea Tajikistan na walifyatua risasi baada ya mabishano ya kidini, shirika la habari la Reuters liliripoti.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy

Tajikistan ni nchi yenye Waislam wengi huko Asia ya Kati. Takriban nusu ya Warrusia wanafuata madhehebu mbalimbali ya Kikristo. Jeshi la Russia lilisema washambuliaji hao walikuwa wanatokea Mataifa Huru ya Jumuiya ya Madola, ambayo ni pamoja na Tajikistan.

Reuters haikuweza mara moja kuthibitisha maelezo ya Arestovych au kupata taarifa ufafanuzi huru wa idadi ya waliouawa au maelezo zaidi ya tukio hilo.

Mashambulizi zaidi ya makombora

Darzeni ya watu nchini Ukraine wameuawa na wengine zadi kujeruhiwa wiki iliyopita wakati majeshi ya Russia yalipopigwa mabomu kwenye miji ya Ukraine kwa kutumia makombora, yakitua katika vituo vya umeme, nyumba za makazi ya watu, barabara kadhaa na maeneo ya michezo.

Kampeni ya karibuni ya kijeshi ya Russia inaonekana ni kulipiza kisasi kufuatia mlipuko wa bomu la kwenye gari wiki moja iliyopita, na kuharibu vibaya sana daraja pekee linalounganisha Russia na Rasi ya Crimea wanayoikalia kimabavu.

Shambulizi katika daraja la Crimean Oct. 8, 2022.
Shambulizi katika daraja la Crimean Oct. 8, 2022.

Hakuna aliyedai kuhusika na shambulizi hilo la bomu.

Jeshi la Ukraine limekuwa likijikita katika juhudi zake kuyakamata tena maeneo ya yaliyotekwa ya kusini na mashariki. Ilitangaza Jumamosi kuwa vikosi vyake vilizima mashambulizi ya Russia karibu na maeneo ya makazi 11.

Ofisi ya Wafanyakazi imeripoti kuwa wanajeshi wa Ukraine walizima jaribio la Russia kusonga mbele karibu na makazi ya watu huko Novosadove, Yakovlivka, Berestove, Bakhmut, Bakhmutske, Opytne, Krasnohorivka, Nevelske, Pervomaiske, Mariinka, na Pobieda katika mkoa wa Donbas.

Maafisa wa Ukraine walisema jeshi lake pia limeshambulia vituo vitano vya kijeshi vya Russia na maeneo yenye wanajeshi wengi wa Russia na kutungua droni sita za Russia.

Msaada zaidi wa Marekani kwa Ukraine

Kusambaa kwa hali hiyo ya mapigano kumekuja wakati Marekani ikitangaza msaada mwingine wa kijeshi kwa Ukraine. White House imeahidi dola milioni 725 katika fungu la usalama kuisaidia Kyiv.

Maafisa wa Marekani walisema fungu hilo la msaada halijumuishi vifaa venye uwezo mpya au vile vya ulinzi wa anga. Badala yake, imejikita katika kuendelea kupeleka mahitaji ya vifaa vya kijeshi na silaha Ukraine ambapo Kyiv imefanikiwa kuvitumia katika kujibu mashambulizi dhidi ya Russia.

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe Biden

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema Jumamosi kuwa licha ya Russia kupeleka majeshi zaidi yakielezwa kuwa ni sehemu ya programu ya kuandikisha wapiganaji iliyotangazwa mwezi uliopita, askari hao inawezekana hawana vifaa.

Rais wa Russia Vladimir Putin alitetea hatua ya hivi karibuni kuongeza mashambulizi katika vita hivyo kwa kupeleka wanajeshi zaidi huko Ukraine.

Rais wa Russia Vladimir Putin
Rais wa Russia Vladimir Putin

Putin alisema Ijumaa hakuna haja ya mashambulizi makubwa mapya dhidi ya Ukraine na kwamba lengo la Russia siyo kuiangamiza nchi hiyo.

Wakati huo huo, kiongozi wa Russia amesisitiza kuwa “hajuti” kuhusu vita hiyo nchini Ukraine na uhamasishaji wa hivi karibuni wa wanajeshi wa akiba wa Russia 222,000 kupigana katika vita hivyo.

Taarifa za mashirika ya habari ya Reuters, AFP na AP zimetumika katika kuandaa repoti hii.

Zinazohusiana

XS
SM
MD
LG