Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 17:03

Iran yakanusha tuhuma za kuipa silaha Russia ili zitumike dhidi ya Ukraine


Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian wakiwa Moscow, Russia, Aug. 31, 2022.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian wakiwa Moscow, Russia, Aug. 31, 2022.

Iran kwa mara nyingine tena imekanusha tuhuma zilizoelekezwa kwao kuwa inawapa Russia silaha mbalimbali “ili zitumike katika vita nchini Ukraine,” wizara ya mambo ya nje ya Jamhuri ya Kiislam ya Iran ilisema Jumamosi.

Kyiv na washirika wake wa Magharibi wameituhumu Moscow kwa kutumia ndege zisizokuwa na rubani (drone) zilizotengenezwa Iran kuishambulia Ukraine katika wiki za karibuni. Suala hilo linatarajiwa kujadiliwa na mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya huko Luxemburg Jumatatu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir- Abdollahian “amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislam ya Iran haijawahi na wala haitatoa silaha zozote ili zitumike katika vita nchini Ukraine,” wizara ya mambo ya nje ilisema katika taarifa yake.

“Tunaamini kuwa kuwapa silaha pande zote zilizopo katika mgogoro zitafanya vita viendelee kwa muda mrefu,” waziri wa mambo ya nje alisema katika mazungumzo yake ya simu na waziri mwenzake wa Ureno Joao Gomes Cravinho.

“Sisi hatujafikiria na wala hatutafikiria vita kuwa ndio njia sahihi iwe Ukraine au Afghanistan, Syria na Yemen.”

Katika mazungumzo mengine ya simu na mkuu wa masuala ya sera za mambo ya nje wa EU Joseph Borrell Ijumaa, Amir Abdollahian amerejea msimamo rasmi wa Iran wa kutofungamana na upande wowote katika vita hivyo ambavyo vilianza miezi takriban minane iliyopita.

“Tunaushirikiano wa ulinzi na Russia, lakini sera zetu kuhusu vita nchini Ukraine siyo kupeleka silaha kwa pande zinazopigana, sisi tunafanya jitihada kusimamisha vita na kumaliza mgogoro wa watu wasiokuwa na makazi.”

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy

Siku ya Jumatatu, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alisema droni za Iran zilitumika katika mashambulizi yaliyofanywa na Russia katika miundo mbinu ya miji kadhaa ya Ukraine.

Mwezi uliopita, Kyiv iliamua kuchukua hatua muhimu kupunguza uhusiano wa kidiplomasia na Tehran kufuatia madai ya nchi hiyo kupelekea silaha mbalimbali Russia.

Iran ilisema uamuzi huo ulikuwa “unamsukumo wa taarifa zisizokuwa na msingi zilizoenezwa na propaganda za vyombo vya habari vya kigeni.”

Mwezi Septemba, Marekani iliiwekea vikwazo kampuni iliyokuwa ikiituhumu inasaidia kusafirisha droni za Iran kwenda Russia ili zitumike nchini Ukraine.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP

XS
SM
MD
LG