Mkutano huo unajiri siku mbili baada ya Russia kufanya mashambulizi ya makombora ya masafa marefu katika miji kadhaa ya Ukraine ikiwemo mji mkuu wa Kyiv.
Mkutano wa Brussels ndio mkubwa kuwahi kuandaliwa na NATO tangu Moscow ilipotangaza kuchukua sehemu za Ukraine na kuziweka chini ya utawala wake, na kutangaza vitisho vya kutumia silaha za nyuklia.
Muungano wa NATO umeitaja hatua ya Russia ni dhihirisho la kuongezeka kwa vita ambavyo vilianza Februari 24, kwa Russia kuivamia Ukraine.
Bomba la mafuta kuelekea Ulaya limeharibiwa
Bomba la mafuta katika bahari ya Baltic limeharibiwa na kuongeza hali ya wasiwasi, japo haijabainika mhusika katika milipuko iliyopelekea uharibifu huo.
Kampuni ya Poland, inayosimamia bomba hilo, ya PERN, imeripoti kugundua kwamba bomba hilo lilikuwa linavuja linalosafirisha mafuta kutoka Russia hadi Ulaya.
Muungano wa NATO umesema kwamba utajibu kwa nguvu zinazostahili iwapo mifumo muhimu ya nchi wanachama itashambuliwa.
Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg ameahidi kuimarisha ulinzi dhidi ya mifumo, akisema kwamba NATO tayari imeongeza wanajeshi wake katika Baltic na bahari za kaskazini.
Ndege za NATO zaidi ya 30, kati hizo kadhaa za kivita na nyambizi chini ya bahari, vinapiga doria.
Akizungumza katika mkutano wa siku mbili na mawaziri wa ulinzi wa muungano huo, Stoltenberg amesema kwamba japo hawajaona mabadiliko yoyote katika mwenendo wa Russia kuhusiana na vitisho vyake vya kutumia silaha za nyuuklia, muungano upo makini sana na utaendelea na mazoezi yake ya kukabiliana na silaha za nyuklia wiki ijayo.
Msaada zaidi wa silaha kwa Ukraine
Muungano wa NATO umeahidi kuendelea kuisaidia Ukraine na silaha za kujilinda angani, siku mbili baada ya mashambulizi ya makombora ya Russia kusababisha vifo vya watu 19, kujeruhi zaidi ya 100 na kuharibu mfumo wa umeme kote nchini Ukraine.
Mfumo maalum wa ulinzi wa anga, unalenga kuzuia mashambulizi ya makombora.
Stoltenberg ameyataja mashambulizi ya makombora ya masafa marefu ya Russia kuwa ishara ya fedheha na dhihirisho kwamba rais Putin anaonekana kuishiwa na maarifa namna ya kuendelea na vita alivyoanzisha.
"Ukweli ni kwamba wameshindwa kupata mafanikio vitani. Russia inashindwa katika vita hivyo,” amesema Stoltenberg akiongezea kwamba "Ukraine inaendelea kukomboa sehemu kadhaa huku Russia ikipoteza na kutumia mashambulizi ya kutisha kabisa dhidi ya raia na kuharibu mifumo muhimu.”
Ukraine imeanza kupata mifumo ya kulinda anga yake dhidi ya makombora
Ujerumani tayari imetoa msaada wa mifumo ya ulinzi wa anga dhidi ya mashambulizi ya makombora.
Kulingana na waziri wa ulinzi wa Ujerumani, moja kati ya mifumo minne ya IRIS-T SLM imeshawasili Ukraine.
Afisa wa ngazi ya juu katika jeshi la Ujerumani, amesema kwamba mfumo wa ujerumani wa IRIS-T, ni ishara kwamba Ujerumani ipo tayari kuisaidia Ukraine kulinda anga yake kutokana na mashambulizi ya makombora ya masafa marefu ya Russia.
Russia, ambayo inataja uvamizi wake nchini Ukraine kuwa “operesheni maalum ya kijeshi” kuwaondoa watkatika hatari na kuwalinda watu wanaozungumza kirusi, imeyashutumu mataifa ya Magharibi kwa kuchochea zaidi vita hivyo kwa kuiunga mkono Ukraine.