Ahadi ya NATO kuisaidia Ukraine imepelekea Russia kuyaonya mataifa ya Magharibi kwamba msaada huo utaiweka NATO katika mgogoro wa moja kwa moja na Russia, na kwamba hatua ya ‘kukubali maombi ya uanachama wa Ukraine katika muungano huo utasababisha vita vya tatu vya dunia”.
Naibu katibu wa baraza la usalama la Russia Alexander Venediktov, ameliambia shirika la habari la Russia TASS, kwamba "utawala wa Kyiv unajua vyema sana kwamba hatua kama hiyo itapelekea kutokea vita vya tatu vya dunia”.
Marekani imeapa kulinda kila sehemu ya nchi washirika.
Utawala wa Moscow umeendelea kutetea hatua yake ya kuivamia Ukraine na kuanzisha vita ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu, ikisema kwamba inafanya operesheni maalum na kwamba nia ya Ukraine kutaka kujiunga katika muungano wa NATO, unatishia usalama wa Russia.
Uanachama wa Ukraine katika NATO
Huenda muungano wa NATO ukachelewesha hatua ya kukubali maombi ya Ukraine kuwa mwanachama wake wakati vita vinaendelea kwa sababu hatua hiyo itaiweka Marekani na washirika wake katika vita vya moja kwa moja na Russia.
Hata kabla ya vita kuanza, NATO ilikuwa imeonyesha dalili za kuchelewesha uanachama wa Ukraine.
Siku chache baada ya Russia kuivamia Ukraine Februari 24, rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alionyesha dalili za kulegeza nia ya nchi hiyo kujiunga na NATO, na kutochukua msimamo wowote.
Lakini muda mfupi baada ya Rais wa Russia Vladimir Putin kutangaza kwamba maeneo ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporizhzhia ni sehemu ya Russia, Sepemba 30, Zelenskiy alitangaza kwamba Ukraine ipo tayari kujiunga na NATO.
Makombora zaidi yanaanguka Ukraine
Zaidi ya sehemu 40 zimepigwa na makombora ya Russia ndani ya saa 24 zilizopita.
Wanajeshi wa Ukraine nao wamepiga sehemu 25 zilizo na wanajeshi wa Russia kwa kuvurumisha makombora 32.
Mji wa Mykolaiv, ulio kusini mwa Ukraine umeshuhudia mapigano makali, Alhamisi.
Gavana wa eneo hilo Vitaly Kim amesema kwamba makao ya watu yamepigwa kwa makombora ya Russia.
Amesema kwamba “jumba la ghorofa 5 linalokaliwa na watu limepigwa na makombora hayo na sehemu yake kuharibiwa kabisa.
Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani zimepiga mji mkuu Kyiv
Russia pia imetekeleza mashambulizi katika mji wa Kyiv kwa kutumia ndege zisizokuwa na rubani. Mifumo muhimu imeharibiwa.
Gavana wa eneo la Kyiv Oleksiy Kuleba, amesema kwamba taarifa za awali zinasema kwamba makombora yaliyotumika yametengenezwa nchini Iran.
Ukraine imeripoti kuongezeka kwa mashambulizi ya makombora yanayotekelezwa na Russia, kufikia 136, katika siku za hivi karibuni.
Iran imekanusha ripoti kwamba inatoa ndege zisizokuwa na rubani kwa Ukraine. Russia haijasema lolote kuhusu ripoti hizo.
Maafisa wa Ukriane wamesema kwamba makombora yamepiga jengo la ghorofa lenye nyumba 30, bomba la mafuta na mifumo ya umeme katika mji wa Nikopol, eneo la Dnipropetrovsk.
Zaidi ya familia 2,000 hazina umeme katika eneo hilo.
Wanajeshi wa Russia wamekuwa wakizidiwa nguvu
Rais wa Russia Vladimir Putin, amesema atatuma wanajeshi 300,000 wa akiba nchini Ukraine, baada ya jeshi lake kupata pigo kubwa tangu mwezi Septemba.
Ametishia kutumia silaha za nyuklia ili kuilinda Russia, na sehemu za Ukraine ambazo amejiingiza kwa nguvu.
Afisa wa ngazi ya juu wa NATO amesema Jumatano kwamba endapo rais wa Russia atatumia silaha za nyuklia, basi “atajibiwa kwa nguvu zinazostahili” kutoka kwa washirika wa Ukraine na ikiwezekana, muungano wa NATO.
Akizungumza mjini Brussels kabla ya mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa nchi wanachama wa NATO, Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin, amesema kwamba "Marekani ipo tayari kulinda mpaka wa kila nchi mwanachama wa NATO endapo itahitajika kufanya hivyo.”
Umoja wa Mataifa wapiga kura kuishutumu Russia
Mjini New York, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa 143 kati ya 193, zimepiga kura ya kulaani hatua ya Russia kujichukulia mikoa minne ya Ukraine.
Syria, Nicaragua, Korea Kaskazini na Belarus ndio nchi pekee ambazo zimeiunga mkono Russia.
China, ambayo ni mshirika mkubwa wa Russia, imesusia kura hiyo.
Mjini Brussels, zaidi ya nchi 50 zilikutana Jumatano na kuahidi msaada zaidi wa kijeshi kwa Ukraine, hasa mfumo wa ulinzi wa anga, baada ya Putin kuamuru mashambulizi ya makombora kufuatia kuharibiwa kwa daraja linalounganisha Russia na Crimea.
Kati ya nchi ambazo zimeahidi msaada wa silaha kwa Ukraine ni Ufaransa, Uingereza na Canada.
Watu 26 wamefariki kutokana na mshambulizi ya makombora ya Russia nchini Ukraine wiki hii.
Waziri wa uUinzi wa Marekani Austin, ameyataja mashambulizi ya Russia kuwa “uovu na ukatili”.