Baraza hilo liliidhinisha azimio hilo huku mataifa 143 yakiunga mkono na matano yakipinga, lakini mataifa 35 yalijizuia zikiwemo China, India, Afrika Kusini na Pakistan, licha ya juhudi kubwa za kidiplomasia za Marekani kutaka Moscow kulaaniwa kwa uwazi.
Azimio "liliilaani hatua ya Russia ya kile kinachoitwa kura ya maoni ndani ya mipaka inayotambuliwa kimataifa ya Ukraine" na "jaribio la kunyakua maeneo hayo kwa njia haramu" lililotangazwa mwezi uliopita kuhusu mikoa minne na Rais Vladimir Putin.
Linatoa wito kwa mashirika yote ya Umoja wa Mataifa na kimataifa kutotambua mabadiliko yoyote yaliyotangazwa na Russia.
"Kura hiyo ilionyesha Russia kwamba haiwezi kufuta taifa huru kutoka kwenye ramani," Biden alisema katika taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani.