Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:13

Kim Jong Un ajitokeza katika uzinduzi wa kıwanda cha mbolea


Shirika la habari la Korea Kaskazini (KCNA) Mei 2, 2020 lilichapisha picha ya Kim Jong Un wa pili kulia akikagua kiwanda cha mbolea jimbo la kusini la Pyongyang Korea Kaskazini. (Photo by S
Shirika la habari la Korea Kaskazini (KCNA) Mei 2, 2020 lilichapisha picha ya Kim Jong Un wa pili kulia akikagua kiwanda cha mbolea jimbo la kusini la Pyongyang Korea Kaskazini. (Photo by S

Baada ya wimbi la habari za uvumi kuwa kiongozi wa Korea Kaskazini ni mgonjwa sana au amekufa, Kim Jong Un ameibuka hadharani kwa mara ya kwanza baada ya siku 21.

Mahala alipochagua kiongozi huyo kujitokeza tena ni eneo lisilo na mvuto : ni tafrija ya kumalizika ujenzi wa kiwanda cha mbolea huko Sunchon, mji ulioko kilomita 50 kutoka jiji kuu la Pyongyang.

Televisheni ya taifa ilimuonyesha akitabasamu, akivuta sigara na kuongea na maafisa wa ngazi ya juu wakati akikagua kiwanda hicho. Japo kuwa katika baadhi ya nyakati alikuwa akichukuliwa na gari ndogo inayotumiwa na wacheza golf, lakini Kim hakuonyesha dalili za waziwazi kuwa ana tatizo la kiafya.

Watu wakitizama televisheni wakati kiongozi Kim alipojitokeza kwa mara ya kwanza May 2, 2020
Watu wakitizama televisheni wakati kiongozi Kim alipojitokeza kwa mara ya kwanza May 2, 2020

Minong’ono kuhusu afya yake Kim ilianza pale habari kuenea kwamba hajajitokeza katika maadhimisho makubwa ya kisiasa ya, siku ya kuzaliwa babu yake Kim Il Sung Korea yanayofanyika kila mwaka Aprili 15. Sababu za kutoshiriki katika maadhimisho hayo, ya muanzilishi wa Korea Kaskazini ya leo bado hazijulikani, na vile vile wakati wa uamuzi wake wa kujitokeza tena hadharani.

“Ni bora nisitoe maoni hivi sasa juu ya hilo,” Rais wa Marekani Donald Trump amesema Ijumaa. “Tutakuwa na la kusema juu ya hilo katika wakati muwafaka.”

Hii siyo mara ya kwanza kumekuwa na uvumi juu ya hali ya afya ya Kim. Mwaka 2014, Kim alitoweka katika matukio ya umma kwa takriban siku 40, na kuzuwa kila aina ya uvumi. Hatimaye alijitokeza tena akitembea kwa kutumia bakora.

Lakini katika kipindi hiki uvumi huo ulikuwa mkubwa, na hoja zinazotafautiana pia.

Katika zilizojitokeza : Kim alikuwa amefanyiwa upasuaji wa moyo ulokua na matatizo na kusababisha kifo chake, alikuwa amezuiliwa nyumbani kwa sababu ya hofu ya virusi vya corona au alijeruhiwa kutokana na uzembe ulitokea katika jaribio la makombora.

Tovuti ya TMZ, inayozungumzia udaku kuhusu watu mashuhri mbalimbali duniani, iliripoti kuwa Kim ameaga dunia.

Katika mitandao ya kijamii, suala la kifo cha kiongozi wa Korea Kusini likawa ni utani wa mitandao, kukiwa na hashtag inayosema #KimJongUnDead ikivuma katika Twitter, Instagram na mitandao mengine.

Maafisa wa Korea Kusini walitupilia mbali ripoti hizo, wakisisitiza kuwa Kim yungali hai na anaendelea kutawala nchi hiyo ya Korea Kaskazini.

Baadhi ya maafisa mjini Seoul walisema Kim inawezekana alikosekana katika sherehe za kila mwaka Aprili 15 kwa sababu ya hofu ya virusi vya corona.

Korea Kaskazini imesema kuwa haina maambukizi yoyote ya virusi vya corona nchini humo, madai ambayo wataalam wanasema siyo rahisi hilo kuwa kweli.

Katika picha ya video iliyochapishwa na kituo cha habari cha taifa Jumamosi, siyo Kim wala maafisa wa ngazi ya juu waliokuwa wamemzunguka walikuwa wamevalia maski usoni.

Lakini wengi kama siyo watu wote waliobakia waliojitokeza katika tukio hilo walikuwa wamevalia maski katika kundi la mamia waliojitokeza kwenye tafrija hiyo ya ufunguzi wa kiwanda cha mbolea.

Kim mwenye umri wa miaka 36 anaonekana ameongeza uzito tangu kuchukuwa madaraka kutoka kwa baba yake Kim Jong II baada ya kuaga dunia mwaka 2011.

Afya ya Kim ni kitu cha kuzungumziwa kwa sababu hana mrithi anayejulikana, hivyo afya yake kuleta wasiwasi juu ya mvutano wa madaraka katika nchi yenye kujihami na silaha za nyuklia.

“Kuyumba kwa Korea Kaskazini na matatizo ya kupokezana madaraka ni jambo linaweza kutokea, na sisi lazima tuwe tumejitayarisha,” anasema Mintaro Oba, mwanadiplomasia wa zamani wa Marekani anayefuatilia masuala ya Korea.

Lakini tukio hili linatukumbusha ni kwa ufinyu gani tunafahamu harakati za viongozi wa ngazi ya juu wa Korea Kaskazini, “nchi yenye siri zaidi kuliko nchi nyingine yeyote zenye kuweka siri,” anasema Bruce Klingner, afisa wa zamani wa CIA kuhusu masuala ya Korea.

XS
SM
MD
LG