Rais wa Marekani Donald Trump alisema Jumatano kwamba alipokea barua nzuri kutoka kwa Kim Jong Un na huenda atakutana na kiongozi huyo wa Korea kaskazini katika siku zijazo.
Trump alieleza katika mkutano wa baraza la mawaziri huko White House kwa "tumeendeleza uhusiano mzuri sana”. Huwenda tukawa na mkutano mwingine. Matamshi ya Rais Trump yamekuja siku moja baada ya Kim kuonya kuwa nia njema ya sasa na Marekani inaweza kumalizika kama Washington itaendelea kuweka vikwazo kuilazimisha serikali yake kuachana na harakati za nyuklia.
Katika hotuba yake ya mwaka mpya Kim Jong Un alisema ilikuwa nia yake thabiti kwamba Korea kaskazini kamwe haitatengeneza tena au kufanya majaribio ya silaha za nyuklia, au kutumia au kusambaza silaha zake.
Kim aliongeza kwamba alikuwa yuko tayari kufanya mkutano mwingine na Rais wa Marekani Donald Trump mwaka huu. Lakini alisema nchi yake itachukua njia nyingine mpaka Washington ichukue hatua za majibu kwa suala hili.
Kiongozi huyo wa Korea kaskazini aliitaka Marekani na Korea kusini kuacha mazoezi yote ya pamoja ya kijeshi.