Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 07:02

Mkutano wa Trump, Kim Vietnam : Nini kitakachojadiliwa?


Mwanamke akipita mbele ya matangazo ya mkutano wa Marekani na Korea Kaskazini katika kituo cha vyombo vya habari vya kimataifa Hanoi kuanzia Feb. 27 na 28.
Mwanamke akipita mbele ya matangazo ya mkutano wa Marekani na Korea Kaskazini katika kituo cha vyombo vya habari vya kimataifa Hanoi kuanzia Feb. 27 na 28.

Mwaka 2018 huko Singapore, Donald Trump na Kim Jong Un walikubaliana kushirikiana katika “kutokomeza kabisa silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea.” Wiki hii mjini Hanoi, wanakabiliwa na kazi ngumu zaidi : kukubaliana na tafsiri ya kutokomeza silaha za nyuklia na kutafuta njia ya kupeleka mbele mchakato huo.

Haya ndio ya kutupia macho wakati wa mkutano wa Trump na Kim huko Vietnam.

Je, mkutano wa Hanoi unaweza kumaliza uhasama?

Kufuatia mkutano wake wa kwanza na Kim, Trump ametangaza “hakuna tena tishio la nyuklia” kutoka Korea. Baada ya miezi nane, Marekani na Korea Kaskazini zinaonekana kupiga hatua ndogo katika suala la nyuklia, na kumekuwa na shinikizo zaidi likimtaka Trump kuonyesha matokeo.

Mpaka hivi karibuni, Korea Kaskazini ilikuwa haikubali kufanya mazungumzo endelevu ya ngazi ya chini kabisa. Wakati mkutano wa Hanoi ukikaribia, hali imebadilika. Maafisa wa Marekani na Korea Kaskazini wamekwisha fanya mikutano siku kadhaa huko Hanoi kabla ya kuwasili kwa Trump na Kim.

Je, pande zote mbili zinaweza kuwa na muono wa pamoja juu ya nyuklia?

Wiki iliyopita, afisa wa Marekani alikiri kuwa Korea Kaskazini na Marekani bado wanajaribu kufikia muwafaka juu ya tafsiri ya kutokomeza silaha za nyuklia – ambayo ni dhana inayokanganya na haina tafsiri ya kiufundi.

Kwa upande wa Washigton, kuondoa silaha za nyuklia inamaanisha Korea Kaskazini itokomeze silaha zake zote za nyuklia. Kwa Pyongyang, jambo hilo ni suala tete.

Korea Kaskazini inapendelea tamko la “kuondoa silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea.” Kwa Pyongyang, fikra hiyo kwa kawaida imehusisha Marekani kuondoa au kupunguza makubaliano yake ya kuwalinda washirika wake, ikiwemo Korea Kusini.

Ili kuondoa mkanganyiko huo, maafisa wa Marekani wanamatumaini kuwa mkutano wa Hanoi utamalizika kwa kupatikana “muongozo” utakaoweka matarajio ya pande zote mbili. Haijulikani vipi waraka huo wa kuonyesha njia ya kufikia makubaliano hayo utaafikiwa na iwapo utakuwa na muda maalum wa kufikia malengo hayo.

Je, Kim atakubali kufanya mchakato huo wende mbele?

Ripoti zinaeleza kuwa Korea Kaskazini inaweza kupendekeza hatua chache za kuondoa silaha zake za nyuklia ikiwa ni ushahidi wa nia yake ya kutokomeza silaha za nyuklia.

Hilo inaweza kuwa pamoja na kukubaliana na kadhia ya kuondoa angalau sehemu ya kituo cha nyuklia cha Yongbyon au vituo vyake vingine vya nyuklia.

Wakati Yongbyon haiwakilishi programu nzima ya nyuklia ya Korea Kaskazini, “hata hivyo ni sehemu kubwa ya programu hiyo,” amesema Robert Manning, afisa wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani aliyejikita katika masuala ya Korea.

Hatua nyengine zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na kukabidhi baadhi ya makombora au silaha za nyuklia, na pia kutoa orodha ya vituo vya nyuklia na makombora, kuwaruhusu wakaguzi wa kimataifa kuingia na kuchunguza katika vituo hivyo.

Je, Marekani itaondoa vikwazo?

Uongozi wa Trump kwa muda mrefu umekuwa ukisisitiza kuwa hautalegeza vikwazo mpaka pale Korea Kaskazini itakapotokomeza kabisa programu yake ya nyuklia. Lakini hivi karibuni, White House inaonekana kulegeza msimamo wake.

Katika mahojiano siku ya Jumapili na shirika la habari la CNN, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo amesema Washington inaweza kuondoa baadhi ya vikwazo dhidi ya Korea iwapo itachukuwa “hatua muhimu,” ingawaje amesisitiza kuwa “vikwazo vya msingi “ vitaendelezwa.

Uwezekano moja wa makubaliano : Marekani inaweza kuruhusu kuanza upya miradi ya pamoja ya Korea ambayo itaweza kuipatia Korea fedha za dharura, ikiwemo eneo la viwanda la Kaesong, upande wa kaskazini wa eneo lililokuwa halina harakati za kijeshi na eneo la utalii la Mount Kumgang lililokuwa Kaskazini.

Je, Vita ya Korea vinaweza kumalizika?

Maafisa wa Marekani wanafikiria iwapo watumie mkutano huo kutangaza kumalizika rasmi kwa vita vya Korea, ambavyo vilifikia kusitisha mapigano zaidi, kuliko kufikiwa makubaliano ya maktaba wa amani mwaka 1953.

Japokuwa tamko hilo litakuwa zaidi ni la ishara, pengine Marekani inaweza kukataa kutoa tamko hilo mpaka pale Korea Kaskazini itakapochukuwa hatua zaidi kutokomeza silaha za nyuklia.

Kwa sababu kumaliza rasmi vita vya Korea kutadhoofisha shinikizo la kimataifa dhidi ya Korea Kaskazini na kuibuwa maswali kuwa wanajeshi wangapi wa Marekani wanahitajika Korea Kusini.

Je, jeshi la Marekani litasita kuwepo Korea Kusini?

Wakati wa mkutano wake yeye na Kim huko Singapore, Trump alikubali kusitisha mazoezi ya pamoja ya kijeshi yanayofanyika kwa kushirikiana na Korea Kusini. Trump anaweza kuamua kufanya maamuzi kama hayo wakati akikutana yeye binafsi na Kim huko Hanoi.

Trump na maafisa wengine wa ngazi ya juu wa Marekani wamesisitiza kuwa kuondolewa au kupunguzwa idadi ya majeshi ya Marekani haitakuwa ni sehemu ya mazungumzo ya nyuklia. Lakini Trump ana historia ya kuhoji ufanisi wa jeshi hilo na gharama za kulihudumia jeshi la Marekani lenye askari 28,000 huko Korea.

Je, Trump na Kim watakabidhi mazungumzo hayo kwa wanasayansi?

Moja ya mafanikio makubwa ya Mkutano wa Hanoi itakuwa kukabidhi mazungumzo hayo kwa wanasayansi, anasema James McKeon, mchambuzi wa sera katika kituo cha udhibiti wa silaha za nyuklia.

McKeon anasema : "Viongozi hao wawili wa nchi hizo hawawezi kutatuwa jambo lolote wenyewe," Sidhani wanauelewa wa kutosha kuweza kusimamia baadhi ya masuala haya nyeti ambayo unahitaji mwanasayansi kuyasimamia, utahitaji wataalamu wenye ujuzi wa masuala haya.

Trump, ambaye amekuwa akisifu mafanikio ya mahusiano yake na Kim, amesema wiki iliyopita anamatumaini ya kuwepo mikutano mingi zaidi na kiongozi wa Korea Kaskazini siku za usoni.

XS
SM
MD
LG