Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 20:57

Ghuba ya Uajemi : Kamanda asema bado Iran ni tishio kwa majeshi ya Marekani


Jenerali. Kenneth "Frank" McKenzie
Jenerali. Kenneth "Frank" McKenzie

Iran imechaguwa “kurudi nyuma na kutafakari” baada ya kufanya matayarisho kufanya kile kilichokuwa kinaonekana kuwa ni hatua ya kushambulia majeshi ya Marekani katika eneo la Rasi ya Uajemi.

Hata hivyo jeshi la Marekani linasema ni mapema mno kusema kuwa hatari hiyo imetoweka, kamanda wa ngazi ya juu wa vikosi vya Marekani huko Mashariki ya Kati amesema Alhamisi.

Katika mahojiano na waandishi watatu wakiwa wamefuatana naye katika ziara yake ya Rasi hiyo, Jenerali Frank McKenzie amesema bado ana wasiwasi juu ya uwezekano wa Iran kufanya vitendo vya uchokozi, na bado anafikiria kuomba vikosi zaidi ili kuimarisha ulinzi dhidi ya makombora ya Iran au silaha nyingine.

“Na wala Siamini kuwa tishio hilo limepungua,” McKenzie amesema, “ Na amini tishio hilo ni la uhakika.”

McKenzie, mkuu wa Central Command ya majeshi ya Marekani, na maafisa wengine wa jeshi wanajaribu kuweka uwiano kati ya kuishawishi Iran kuwa Marekani imejiandaa kulipiza kisasi kwa shambulizi dhidi ya Wamarekani, na hivyo kuzuia vita, na kuweka shinikizo la nguvu za kijeshi katika Rasi hiyo, inapelekea Iran kufikiria kuwa Marekani inapanga kuishambulia, hali ambayo inaweza kuisukuma Iran kushambulia kuzuia shambulizi dhidi yao na hivyo kuzusha vita.

Mvutano kati ya Marekani na Iran umefikia hali mbaya sana tangu Rais Donald Trump alipojiondoa kutoka katika mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa kadhaa yenye nguvu, na kurejesha vikwazo dhidi ya Tehran.

Mwezi uliopita, kwa kujibu kile kilichoelezwa na maafisa wa Marekani kama ni tishio linalofukuta, Marekani ilitangaza kupeleka manwari yake inayobeba ndege za kivita na silaha nyingine katika eneo la Rasi hiyo.

Marekani pia imeilaumu Iran kwa shambulizi la mwezi uliopita lililolenga meli za mafuta katika bandari ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Siku ya Alhamisi, mabalozi wa Umoja wa Mataifa kutoka UAE, Saudi Arabia na Norway wamewaambia wajumbe wa Baraza la Usalama kuwa wachunguzi wanaamini mashambulizi hayo yaliendeshwa na taifa la kigeni likitumia wazamiaji waliokuwa katika boti za mwendo kasi walioweka mabomu katika meli hizo. Lakini hawakuitaja Iran.

Hapo awali, balozi wa Saudi Arabia katika UN, Abdallah Al-Mouallimi, amesema Saudi Arabia inailaumu Iran kwa hujuma ya meli hizo.

Akiwa mjini Baghdad, McKenzie amewaambia waandishi wa habari wa shirika la habari la The Associate Press na mashirika ya habari mengine mawili kuwa kupelekwa tena kwa majeshi ya Marekani katika Rasi hiyo “imesababisha Wairan kurudi nyuma kidogo, lakini sina uhakika iwapo wanarudi nyuma kimkakati.”

Jenerali huyo amesema Marekani inaonyesha nguvu ya kutosha kuweza “kuweka kizuizi” bila ya “kuwepo ulazima” wa kuwachokoza maadui wake wa muda mrefu.”Tunajaribu kadiri tuwezavyo kujizuia.

XS
SM
MD
LG