Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 06:59

Netanyahu : 'Wananchi wa Iran sio maadui zetu, ni marafiki zetu'


Benjamin Netanyahu
Benjamin Netanyahu

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alizungumza Alhamisi na Mwandishi wa Sauti ya America -VOA huko mjini Warsaw, Poland na kufafanua namna Israeli inavyofanya mawasiliano na nchi za Kiarabu na juu ya mkataba wa nyuklia wa Iran uliofikiwa na mataifa ya Magharibi.

Netanyahu alikuwa Warsaw kuhudhuria Mkutano unaoongozwa na Marekani juu ya usalama wa Mashariki ya Kati.

Swali : Baada ya Mkutano huu, je, umefanikiwa kuzishawishi nchi za Ulaya kuwa na mtizamo wako na pia msimamo wa Rais Donald Trump juu ya Iran, au tuseme, kupata ushirikiano?

Waziri Mkuu : Bila shaka, nafikiri kitu muhimu sana kilitokea, kwa sababu kulikuwa kwa mara ya kwanza, na mawaziri wa mambo ya nje 60 kutoka nchi 60, na mawaziri wa mambo ya nje kadhaa kutoka nchi za Kiarabu, na waziri mkuu wa Israeli, mimi mwenye, ni mara ya kwanza, kukutana nao kwa pamoja. Jambo la pili, kulikuwa na msimamo mmoja kati ya Waarabu na Waisraeli kwamba ni lazima tupambane na vitisho vya utawala wa Iran. Kila mmoja, nikiwemo mimi na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu, tulisema kuwa wananchi wa Iran siyo maadui zetu. Wao ni marafiki zetu. Utawala huu ambao unafanya vitisho dhidi yetu na kuwakandamiza wao pia unawatishia wao. Hili ndio tishio la pamoja ambalo lazima iwepo njia ya kukabiliana nalo, na nafikiri ujumbe huo ulikuwa umesikika wazi na umefahamika vizuri. Nchi za Ulaya, baadhi yao wanakubaliana, kwa namna yoyote ile, lakini iwapo unazungumzia wananchi wa nchi za Magharibi, wamesikia hilo. Je, imekuwa na athari? Nafikiri imekuwa na athari kwao. Haimkiniki kuwa wanashindwa kuona kuwa Waarabu na Waisreali wanakubaliana, na pale Waarabu na Waisraeli wanapokubaliana juu ya jambo lolote, unajua, nafikiri inabidi watu wa Ulaya wasikilize. Hivi sasa, najua kuwa wananchi wa Iran wanatusikiliza, kwa sababu najua kuwa kila wakati ninapoongea na umma wa Iran na picha za video zinazosambazwa baadhi ya wiki, ninapokea majibu yenye kusisimua. Na hivyo kwa kweli, nafikiri ulimwengu wa Kiarabu hivi sasa kwa kiwango kikubwa wako pamoja na Israeli katika msimamo wake. Marekani, iko pamoja na sisi, na inawezekana wananchi wengi wa Iran wako pamoja katika msimamo wetu. Pengine watu wa Ulaya wao wako nje ya mstari, unajua, hawajakuwa na msimamo. Kama tunavyosema katika mchezo wa mpira wa miguu, wameotea.​

Swali : Waziri Mkuu kwa ruhsa yako, nitarejea katika suala la mawasiliano uliyokwisha fanya, mawasiliano yako na wananchi wa Iran, na pia umegusia umoja uliokuwepo na ulimwengu wa Waarabu au baadhi ya mataifa ya Kiarabu. Hilo lilifanyika lini? Kwa sababu kulikuwa na upinzani huko nyuma kwa nchi za Kiarabu kushirikiana na Israeli.

Netanyahu: Bila shaka, kulikuwa na mchakato hatua kwa hatua wa kurejesha mahusiano. Katika njia mbalimbali tunafanikiwa kushirikiana kwa pamoja kama ilivyokuwa zamani na Iran. Kabla ya mapinduzi ya Kiislam, tulikuwa na mahusiano mazuri, ushirikiano wa kibiashara, utalii, mafungamano ya kijeshi na mambo mengine, pamoja na kutokuwepo mahusiano kamili ya kidiplomasia. Hilo ndio linalotokea katika nchi mbalimbali, na maeneo mengi ya Ulimwengu wa Kiarabu hivi sasa. Kwanza kabisa bila shaka tumeanzisha mahusiano na mikataba ya amani baina yetu na Jordan na Misri, lakini nchi nyingine hatua kwa hatua tunarejesha mahusiano hayo. Nafikiri tishio la shambulizi kutoka utawala wa Tehran umetufanya tuwekaribu na mataifa mengine, lakini tutakapofikia ushirikiano na mambo mengine yakaanza kutekelezwa, kama vile ushirikiao katika teknolojia, maji, kilimo, nishati, afya – vitu vyote hivi serikali za Kiarabu zinamaslahi navyo, na najua pia vina maslahi na Iran, kwa sababu ninaongea na wananchi wa Iran kuhusu haya. Kwa hivyo linaanza suala la usalama, lakini kinachofuatia ni namna gani hali za maisha kuzifanya ziwe bora zaidi.

Swali : Iwapo utaniruhusu, ninapendelea kukuuliza kuhusu programu ya nyuklia ya Iran. Inavyoonekana kuna tofauti kubwa ya maelezo kati ya Israeli na IAEA (Shirika la Kimataifa la Atomic). Unasisitiza kuwa Iran bado ina vituo vya siri vya nyuklia. IAEA wanasema vituo vyote vimekaguliwa na kuthibitishwa, na kuwa Iran inafuata maagizo ya kimataifa katika kusitisha programu hiyo ya nyuklia. Nani yuko sahihi, na nini sababu kubwa ya tofauti hii?

Netanyahu: Wasiwasi wangu kwa kweli siyo kuwa Iran inavunja makubaliano. Wasiwasi wangu ni iwapo Iran itaendeleza makubaliano haya. Nafikiri makubaliano haya mabaya, kwa sababu yanatoa fursa kwa Iran kufikia silaha za nyuklia. …Iran imepata mabilioni na mabilioni ya dola kwa (kukubali mkataba huu). Fedha hizo zimekwenda wapi? Hazikutumika kwa ajili ya mahospitali, hazikutumika katika kusafisha maji, hazikwenda katika mashule, na wala katika kilimo. Zimetumika – Nitakwambia zimekwenda wapi : Kwa sababu ya mkataba huu, sawa, zimekwenda kuwasaidia waasi wa Houthi, zimekwenda kwa kikundi cha Hezbollah. Zimekwenda Iraq, zimekwenda Syria kwa vikundi vya wanamgambo wa Kishia.

Fedha hizi hazikuwafikia watu wa Iran. Kwa hiyo, unajua, nafikiri hili ni jambo baya… Israeli inapata mafanikio. Inakuwa kwa sababu tunao uchumi uliowazi na imara. Iran, ingeweza kuwa ni historia yenye mafanikio, kwa njia nyingi, katika sehemu hii ya ulimwengu. Iran haina maji. Unajua, watu wanagharama mbalimbali za maisha, na wanakosa mahitaji mengi. Kwa nini? Kwa sababu utawala huu haujali watu wake. Unachukuwa fedha kwa kujinufaisha wenyewe au unatumia kwa ajili ya kuvamia nchi nyingine, na bila shaka Waarabu na Waisraeli wanakubaliana kupambana dhidi ya uvamizi wa Iran unaoelekezwa kwa mataifa ya Kiarabu—lakini kwanza ni kwa Waislam. Na unatambua kuwa uvamizi huo ni wa namna mbaya kabisa, lakini ukandamizaji huo pia unaelekezwa dhidi ya wananchi wa Iran wenyewe. Na wananchi hao wanajitokeza kuandamana, na unajua, maramoja wanapigwa na kunyanyaswa. Lakini watu lazima waulize swali la kawaida. Makubaliano ya nyuklia yametoa fursa ya utajiri na fedha nyingi. Uko wapi utajiri huo? Fedha hizo ziko wapi? Kwa nini wananchi wa Iran wanapata tabu? Kwa sababu utawala huu unafuja fedha hizo kwa ajili ya uvamizi nchi nyingine.

Swali : Umetaja kikundi cha Hezbollah. Nataka kukuuliza juu ya vikundi vingine vinavyoiwakilisha Iran katika eneo. Je, unafikiri kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya vikundi hivi, kwa sababu ya fedha zinazoingia nchini Iran, vitaweza kudhoofisha operesheni za vikundi hivi dhidi ya Israeli wakati fedha zitakapotoweka?

Netanyahu: Bila ya shaka fedha zinakauka. Tunaliona hilo. Kusitishwa kwa fedha hizi inamaanisha kuwa lazima wakate misaada yao kwa Hezbollah, Wahouthi na Hamas – “makundi hayo matatu yanayoanzia na herufi H” – lakini pia Syria hawatoi tena fedha kwa sababu haziko. …Lakini bado wanatoa fedha (kwa) vikundi vinavyoiwakilisha na vinginevyo, lakini … hivi sasa wanazo fedha kidogo za kugawa.

Swali : Hivi sasa nchini Syria, Israeli inavishambulia vituo vya Iran huko Syria. Je, hili limekuwa na mafanikio makubwa kama operesheni ya kijeshi na kwamba hivi sasa mko vitani na Iran?

Netanyahu: Angalia, Iran inasema kuwa wanataka kulifuta taifa la Kiyahudi la Israeli. Inasema kuwa inataka kuiangamiza Israeli. Waziwazi, kila siku, kila baada ya masaa mawili. Sawa, kwa hiyo wanasema kuwa wanataka kuleta sehemu kubwa ya jeshi lao na vifaa vyao vya kisasa vya kijeshi na wanamgambo wa Kishia – ambalo linawapiganaji zaidi ambao sio Wairan, na hivyo – katika mlango wa Israeli, umbali wa kilomita 1,500. Nini ninatakiwa kufanya? Kuna mtu anasema, “Tutawauwa, tutaiangamiza nchi yenu. Na tutaleta silaha na mbinu za kufikia malengo yetu,” na hivyo nikasema hapana. Hatutaruhusu hilo kutokea. Na ikitulazimu, sisi, wewe unajua, iwapo watajaribu kuweka vituo vya kijeshi jirani na mpaka wetu kwa minajili ya kutuangamiza, sisi tutazuia hilo. Tulikuwa tunafanya hivyo, na je, imekuwa na mafanikio? Kwa kiwango kikubwa, ndio, lakini sio kikamilifu. Na maana, bado wako pale, lakini wangelikuwa wamejiimarisha zaidi kama tungekuwa hatujachukuwa hatua. Kwa kweli, uwepo wao umepungua kwa kiwango fulani.

Swali : Umekuwa ukiwaonya viongozi wa dunia juu ya hatari za programu ya makombora ya balistik ya Iran. Je, umezungumza na viongozi wa dunia kile Iran wanachokifanya waziwazi, kutaka “Israel iangamie” na vitisho vya makombora yake, (na) nchi gani itafanya hivyo iwapo inataka kuwa mwanachama mwenye kuwajibika katika jumuiya ya kimataifa. Je umezungumza na viongozi wa mataifa mengine juu ya hilo?

Netanyahu : Naam, mara nyingi, lakini pia nimezungumza nao kuhusu wao, kwa sababu Iran imekuwa ikiuwa kwa mpango maalum raia wa Iran, wapinzani ambao wanamaoni tofauti. Wananchi wanataka kuona Iran iliyo huru, yenye demokrasia; wanataka kuona Iran inakuwa ni nchi inayoweza kutumia uwezo wake kikamilifu. Na watu hawa ambao wanaishi katika miji mikuu ya nchi mbalimbali za Ulaya wanauawa kwa mpango maalum. Hivyo tumeweza kugundua baadhi ya hila hizi. Tumezuia baadhi ya hila hizi, hawa wauaji wa wananchi wa Iran, kuweza kufanya mauaji haya katika miji mikuu ya Ulaya. Kwa hiyo, nimewataka viongozi wa Ulaya kunambia, katika wiki ambazo tulikuwa tumewaonyesha mpango wa mauaji katika nchi zao wenyewe, bado mnakutana na wawakilishi wa utawala wa Iran kuwasaidia wakwepe vikwazo vya Marekani, mnajua hili, angalau basi muwe mnajiheshimu na kuweka msimamo. Vipi mnaweza kufanya hili? Nafikiri nchi za Ulaya ni lazima litizame upya mwenendo wanaochukuwa kwa utawala na Tehran. Nafikiri madikteta wa Tehran wasiruhusiwe kukanusha mauaji. Kiukweli, ni uvamizi wao wa kikatili katika eneo, na kile wanachowafanyia watu wao wenyewe. Kile wanachokifanya na kuwanyima haki zao kunawafanya wananchi wapate tabu Iran. Na kama nilivyosema, nimeongea na watu wa Iran, nimeongea juu ya kubadilishana ujuzi katika masuala ya maji, ukweli kuwa tulipeleka watu kusaidia waathirika wakati wa tetemeko la ardhi. Kwa kuwa tunauwezo wa kusaidia katika kilimo na tunaweza kusaidia kitu chochote – na maanisha, uwezekano wa yale tunayoweza kusaidiana pamoja hauna kikomo. Hauna kikomo, unajua hilo, wakati hilo linaendelea hivi sasa, linaendelea pia katika nchi za Kiarabu, fikiria hilo? Huko nyuma tulikuwa maadui wakubwa, na hivi leo, unajua, inakuwa ni uhalisia mwengine. Inaweza kuja kutokea hivyo hivyo kwa Iran, na wananchi wa Iran wanaweza kuja kuwa na maisha mazuri, lakini siyo chini ya utawala huu.

Swali : Umewataja mara kadhaa wananchi wa Iran. Nataka kupata maoni yako juu ya maandamano yanayoendelea nchini Iran na kile unachotabiri kinaweza kutokea.

Netanyahu: Nafikiri kitu chakuvutia ni kuwa, unajua watu walisema, “ Bila shaka, nchi haina uongozi,” na nikwaambia ni jambo la kufurahisha, kwa sababu inamaana kuwa udhaifu huo ni kutoka ngazi ya chini hadi juu, na kuwa haina mpangilio Madhubuti. Na kuwa watu wake wanataka kuwa huru. Wananchi wa Iran ni wenye vipaji. Ni watu ambao wanaurithi mkubwa wa kihistoria katika tamaduni zao. … Ukisoma juu ya ustaarabu mkuu uliokuwa miaka 2,500 iliyopita, sisi katika Bibilia – katika Bibilia ya Kiyahudi, tunamzungumzia Mfalme Cyrus kama ni moja wa viongozi mashuhuri wa historia yetu. Tunavutiwa na uongozi wake na urafiki aliyouonyesha kwa Wayahudi. Kwa hiyo bila shaka, Iran inautamaduni uliotukuka ambao tunautambua katika historia yetu, na bila shaka watu wa Iran na Wafursi, wanaijua historia yao. Iran inastahili kufikia hali nzuri zaidi. Watu kama hao wenye vipaji na utamaduni wenye kujitosheleza, wanastahili kuwa na hali nzuri sasa na pia wanastahili maisha mazuri baadae. Lakini maisha bora hayawezi kupatikana, unajua, chini ya madikteta wa kidini ambao walichukuwa nchi na kuiangamiza. Angalia pato letu la taifa (GDP), jinsi lilivyokua, nchini Israel. Wakati wa miaka 40 ya mapinduzi ya Iran, angalia kitu gani kilitokea. Iran ilitakiwa iwe mbali sana. Hivi sasa imeanguka chini. Na nafikiri ni juu ya watu wenyewe wanaotaka kufanya maamuzi kufanya wanalotaka na utawala huu. Nafahamu maandamano yao. Na nafahamu ushupavu wa watu kujitokeza mabarabarani au kwenda katika mtandao wangu wa Facebook, inataka ushupavu. Wanafanya hivyo, inamaana kwamba hawajakata tamaa.

Swali : Waziri Mkuu, ikiwa ni swali la mwisho, je, unaweza kutuambia juu ya athari za kampeni na mawasiliano yako katika lugha ya Kifarsi. Si maanishi wewe binafsi lakini kituo chako, mtandao wa YouTube na Twitter?

Netanyahu: Naam, naweza kukwambia kile wataalam walichonambia, kwa sababu naweza kueleza na angalia, unajua, athari za tathmini za haraka, kwa kusikiliza kile watu wanachoandika, wanachosema na mengineyo. Lakini nina watu ambao walifanya tathmini juu ya hilo na wamesema kuwa tumeweza kuwafikia watu wengi katika maeneo tofauti na ya mbali nchini Iran, na hilo linaridhisha sana. Kwangu mimi, hii ni ishara ya matumaini. Hii ni ishara ya matumaini, kwa sababu ina maana kwamba watu wa Iran hawakubaliani na propaganda za utawala wa Iran. Wao ni mahiri zaidi ya hizo propaganda. Na bila shaka kwa kuwa wanawasiliana na waziri mkuu wa Israeli na kuonyesha kumuunga mkono, kitu ambacho kinahitaji ushajaa wa kipekee, hilo linanijulisha kuwa Iran inamustkbali wenye mafanikio makubwa.

XS
SM
MD
LG