Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kutangaza katika siku kadhaa zijazo kwamba hatoidhinisha tena kwamba Iran inatekeleza mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 na kulipa bunge siku 60 kuamua kama kuna haja ya kurejesha tena vikwazo vya Marekani kwa Tehran. Kufuatana na sheria rais ana hadi Oktoba 15 kuamua lakini vyanzo vya Ikulu ya Mrekani-White House vinasema huwenda suala hili likatokea mapema zaidi.
Msemaji wa White House, Sarah Huckabee Sanders alisema Jumanne kwamba Rais Donald Trump amefikia uamuzi kuhusu mkakati mzima wa Iran na anataka kuhakikisha kwamba wana sera pana zya kukabiliana na hilo na sio tu sehemu moja ya suala hilo bali kukabiliana na masuala yote ya Iran kuwa ni mshirika mbaya.
Rais Trump aligusia suala hilo mwezi uliopita katika hotuba mbele ya kikao cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Mkataba wa Iran ulikuwa moja ya mikataba mibaya sana ambayo Marekani haijawahi kuifanya alisema.
Uwamuzi wa kutoidhinisha utekelezaji wa Iran hautafutilia mbali mkataba ambao Iran ilifikia pamoja na Marekani na mataifa mengine makuu matano duniani.
Wakati huo huo viongozi wa ulaya akiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May wamekuwa wakiwasiliana na Rais Trump katika siku za karibuni kujaribu kumshawishi kutojiondoa kutoka mkataba. Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza ilieleza kwamba May alimpigia simu Rais Trump siku ya Jumanne kumuhakikishia tena nia ya dhati ya Uingereza kushirikiana pamoja na marafiki zake wa ulaya akisema ilikuwa suala muhimu kwa usalama wa kikanda.